…………………………………………………………………………..
*Awataka wawekezaji watakaotozwa gharama za ziada wasisite kutoa taarifa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Iringa na amesema kwamba Serikali itaendelea kudumisha amani na utulivu ambao ni muhimu kwa wawekezaji na wananchi, hivyo ametoa wito kwa wawekezaji wasisite wa ndani na nje kuwekeza nchini.
Amesema uwekezaji ni tegemeo la Taifa katika kukuza uchumi wake na kuongeza ajira, hivyo serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa Watumishi wa Umma wanaohusika na utoaji wa huduma kwa wawekezaji kwa lengo la kuhakikisha kuwa hawasumbuliwi na pale ambapo hawatohudumiwa vizuri ikiwemo kutozwa gharama za ziada watoe taarifa kwa mamlaka husika.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Januari 23, 2021) alipozindua mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Iringa katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Mkwawa. Alisema mwongozo huo aliouzindua umebainisha vivutio vilivyoko mkoani Iringa ikiwemo mazingira mazuri ya biashara, nguvu kazi, amani na utulivu, maliasili nyingi na soko la kutosha.
“Iringa umejaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji. Hata hivyo, kuwa na fursa ni jambo jema lakini kuwapata wawekezaji makini ni jambo la muhimu zaidi. Wadau mbalimbali hususan wafanyabiashara wanapaswa kuzifahamu fursa hizi kwa kina ili waweze kuja kuwekeza. Mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa vikwazo vyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje.”
Alisema dhamira ya Serikali ni kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta zote na kwamba wawekezaji wakija wawe kama marafiki na wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa na waungwe mkono kwenye maeneo watakayohitaji kuwekeza. “Tuondoe vikwazo visivyo vya lazima na iwapo wamefuata taratibu zinazopaswa, sitegemei kuona wawekezaji wakikwamishwa kutekeleza miradi yao katika kila sekta na kila mkoa.”
Waziri Mkuu alisema kuwa katika kutimiza azma hiyo, watendaji wote wa Serikali katika ngazi mbalimbali wanapaswa kushiriki kutangaza fursa hizo za uwekezaji na pia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta wanazozisimamia ili kurahisisha mazingira ya biashara na uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.
“Katika ziara zangu za mikoani nimesisitiza sana umuhimu wa watumishi wa umma kuwatumikia wananchi wote kwa usawa na bila ubaguzi. Aidha, nimeagiza Wananchi wote na wageni wakiwemo Wawekezaji wanapofika kwenye Ofisi zote za Umma, wapokelewe kwa staha, wasikilizwe na kupewa huduma wanazohitaji kwa uharaka na ufanisi bila urasimu.”
Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka mitano wananchi wameshuhudia jitihada kubwa na za wazi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. John Pombe katika kutoa msukumo wa maendeleo katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii na viashiria vingi vya kiuchumi na kijamii vimeonyesha matokeo mazuri.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa uandaaji wa mwongozo huo wa uwekezaji na amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania wajipange vizuri katika kushindana Kimataifa kwa kuzalisha bidhaa bora.
“Pia wajipange kuelewa mazingira ya uwekezaji hasa kufahamu sheria ambazo zinaongoza uwekezaji nchini ili waweze kuzingatia na kuzitumia ipasavyo. Kwa upande wa Serikali tutatimiza wajibu wetu kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara hapa nchini yanakuwa mazuri sana.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alisema lengo la kongamano hilo la uwekezaji mkoani Iringa ni kuanisha fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Iringa na kuzitangaza ili ziweze kutambulika na kuvutia wawekezaji wengi.
“Tutahakikisha wawekezaji watakaojitokeza hawapati usumbufu na katika kufikia lengo hilo tumeanzisha kitengo malumu kwa ajili ya kuwahudumia wawekezaji katika ngazi ya mkoa kwa kuwapa miongozo muhimu, kuwaunganisha na taasisi zinazotoa huduma, kuwasaidia katika upatikanaji wa vibali kwa wakati na kutatua migogoro baina ya wawekezaji hao na wadau.”
Mkuu huyo wa mkoa aliwahakikishia watu wote wanaohitaji kuwekeza mkoani Iringa wakiwemo na Wana-Iringa wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa zilizopo na kwamba mkoa huo umejipanga ipasavyo kuwahudumia bila ya urasimu wa aina yoyote.
Alisema mwongozo huo uliozinduliwa na Waziri Mkuu pamoja na mambo mengine umebeba dira, maono na muelekeo wao katika kujenga uchumi wa mkoa wa Iringa na unaweka msingi wa kuvutia wawekezaji na kuzalisha ajira za kutosha kwa Wana-Iringa hususan vijana.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa wakati akizindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 13 Novemba, 2020 jijini Dodoma alielezea dhamira ya Serikali ya kutoa kipaumbele katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani na kuvutia wa nje.
Katika hotuba hiyo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa anataka Watanzania wawe mabilionea, hivyo Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kusisitiza kwamba kila Mtumishi wa Umma ashiriki kuwawezesha Watanzania kuwa matajiri kupitia uwekezaji wenye tija ili kutimiza ndoto za Mheshimiwa Rais.