Maafisa utamaduni kutoka Kanda ya kaskazini wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakiendelea na kikao kilichoandaliwa na Basata jijini Arusha(Happy Lazaro)
…………………………………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.Baraza la Sanaa la Taifa limewataka wasanii wote nchini kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kufuata sheria ,taratibu na kanuni na kuepuka ukwiukaji wa maadili .
Hayo yalisema Jana na Mratibu wa shughuli za Sanaa Kanda ya kaskazini,Flora Mgonja wakati akizungumza katika kikao Cha maendeleo ya sekta ya sanaa Kanda ya kaskazini kilichoandaliwa na Basata na kuwashirikisha maafisa utamaduni kutoka Kanda ya kaskazini.
Mgonja alisema kuwa,lengo la mkutano huo ni kuweza kukutana na kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Sanaa ili waweze kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa ili kusimamia maadili.
Alisema kuwa,Basata hawapo kwa lengo la kuwafungia wasanii bali kuweka utaratibu kwa ajili ya kazi zinazofanyika kuhakikisha inafuata utaratibu pasipo kuwepo kwa ukwiukaji wowote wa sheria.
Alisema kuwa, taratibu na sheria za Basata zinamtaka kila msanii kuweza kusajiliwa na akitoa kazi yake yoyote bila kusajiliwa atachukuliwa hatua za kisheria ,hivyo kuwataka kufuata taratibu hizo ili kazi zao ziweze kufanyika kwa weledi mkubwa.
Naye Katibu Mkuu wa umoja wa wanamuziki Tanzania,Stella Joel alisema kuwa,uwepo wa semina hiyo utasaidia sana kuwakumbusha utendaji kazi wasanii hao kwa kushirikiana na maafisa utamaduni na kuweza kufuata sheria na kanuni za kazi zao.
“kwa kweli semina hii inasaidia sana kutukumbusha wajibu wetu katika utendaji kazi huku tukisimamia maadili ya wasanii,na italeta manufaa makubwa Sana kwani ni njia mojawapo ya kuongeza ushirikiano wa karibu Kati ya wasanii na maafisa utamaduni katika kufuata maadili.”alisema Stella.
Naye Afisa utamaduni jiji la Arusha, Elizabeth Ncheye alipongeza viongozi wa Basata kwa kuwakutanisha maafisa utamaduni katika kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa pamoja katika kushirikiana na kuhakikisha maadili yanafuatwa katika wasanii.
Alisema kuwa,kwa kuwakutanisha pamoja kunaongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi katika kuhakikisha kwa pamoja wanasimamia maadili na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wasanii katika utendaji kazi wao.
Kwa upande wake ,Afisa utamaduni jiji la Tanga ,Rose Sempoli alisema kuwa,uwepo wa kikao hicho unawasaidia Sana kuwakumbusha wajibu wao katika utendaji kazi wa kila siku na kuhakikisha sheria na taratibu pamoja na maadili yanafuatwa katika kazi za wasanii .