Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Rehema Nchimbi akimuapisha Bi. Fatuma kuwa Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Singida.
Bw.Yesaya Kindulu akila kiapo.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamimu Hoza akihutubia katika hafla hiyo.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Singida wakiwa kwenye hafla hiyo.
Na Ismail Luhamba, Singida
WAJUMBE wapya wa baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Singida wameagizwa pamoja na mambo mengine wafanye utafiti wa kina kubaini vyanzo vinavyochochea migogoro ya ardhi hasa ndani ya kifamilia.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Rehema Nchimbi baada ya kuapisha wajumbe wanne wa baraza hilo la ardhi na nyumba wilaya ya Singida.
Alisema uzoefu unaonesha wazi kwamba migogoro ya ardhi inayoripotiwa mingi ni kutoka ndani ya familia mbalimbali kila kona mkoani hapa.
“Mkoani kwetu,kaya nyingi zina migogoro ya ardhi.Migogoro ya ardhi,ni sumu mbaya mno.Hatua hiyo husababisha wanafamilia wao kwa wao,kufarakana,upendo kutoweka ,wanafika mahali wanauana… kisa ni ardhi.Hebu kalifanyieni kazi na mtupatie mrejesho, ili tujue undani wake”,alisema.
Aidha Dk.Nchimbi amewaagiza wakuu wa wilaya wote mkoani hapa,wafungue madaftari kwa ajili ya kuweka kumbukumbu mbalimbali ya matukio ya migogoro ya ardhi, kwa kila wilaya na ofisi ya mkuu wa mkoa,itakuwa nao.
“Wakuu wa wilaya ni lazima mtambue kuwa mnawajibika katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inakomeshwa.Migogoro hii inasababisha watu kuuana na wanapoteza muda mwingi kuhagaika na kesi kwenye baraza la ardhi na nyumba.Fuatilieni kila tukio na kulipatia ufumbuzi wa kudumu”,amesisitiza mkuu huyo wa mkoa.
Pia ameagiza watendaji wa kijiji na kata,washirikiane na mkuu wa wilaya,katika kufuatilia matukio mbalimbali ya migogoro ya ardhi.
Aidha Dk.Nchimbi amezitaka familia zenye migogoro ya ardhi wajiepushe na wanasheria uchwara/umiza kwa madai hawajui sheria yoyote kwani wao wanalenga kujipatia fedha na kuwagombanisha watu wachukiane na hata wauane.
Dk. Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe walio kula kiapo na kuwataka waende wakatende haki ili baadhi ya watu wenye migogoro ya ardhi wawe na imani na baraza hilo.
‘Hapa nyuma baraza letu la ardhi limelalamikiwa sana. Ardhi hii imebeba karibu kila kitu ambacho ni muhimu kwa uhai wa viumbe akiwemo binadamu.hivyo wajumbe nendeni mkatende haki…hofu ya Mungu iwatangulie”,alisema.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Anjelina Lutambi aliwataka wajumbe wakafanye kazi kwa weledi mkubwa na bila upendeleo wa aina yo yote ili walalamikaji na walalamikiwa wakiri haki imetendeka.
“Ninyi ni watu muhimu sana,mna unyenyekevu,na mioyo yenu ina huruma.Kazi iliopo mbele yenu ni nzito hivyo mtangulizeni Mungu mbele na kazi yenu ya kutatua migogoro ya ardhi, itakuwa nyepesi “, alisema Lutambi.
Kwa niaba ya wajumbe wenzake,mama Anna Kisenge,alishukuru kwa kuaminiwa kushika jukumu hilo zito na kusema wakati wote watazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na watahakikisha migogoro ya ardhi ilio chini ya uwezo wao wanaipatia ufumbuzi wa kudumu.