Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Juma Kipanga (katikati) akipokea maelezo kutoka kwa msimamizi wa ujenzi wa chuo cha VETA wilaya ya Chemba, Mhandisi Richard Mwakapeje (mwenye kofia nyekundu) wakati alipokuwa akikagua mradi huo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Juma Kipanga akifafanua jambo wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA wilayani ChembaMuonekano wa moja ya majengo yanayojengwa katika chuo cha VETA wilayani Chemba.
*************************************************
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga amewaagiza wasimamizi wote wa miradi ya ujenzi wa vyuo vya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) unaotekelezwa katika Wilaya 25 nchini, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo Machi 31 mwaka huu.
Mhe. Kipanga ameyasema hayo hivi karibuni wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyuo hivyo katika Wilaya za Bahi na Chemba mkoani Dodoma ambapo amesema vyuo hivyo vinatakiwa vikamilike muda huo ili kuruhusu mafunzo kuanza kwa wakati uliopangwa.
“Nawaagiza wasimamizi wote wa miradi ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 25 nchini, kuhakikisha ujenzi wa vyuo hivyo unakamilika ifikapo tarehe 31 Machi mwaka huu ili mafunzo yaweze kuanza kama ilivyopangwa,” amesema Mhe. Kipanga.
Aidha Mhe. Kipanga amewashauri wasimamizi wa ujenzi wa miradi hiyo kutafuta suluhisho mbadala kwa changamoto wanazokutana nazo ili changamoto hizo zisiwe sababu ya kufanya ujenzi huo usikamilike kwa wakati.
“Iwapo muuzaji wa vifaa mfano mabati, nondo au sementi anashindwa kuwaletea vifaa hivyo kwa wakati, tafuteni muuzaji mwingine atakayeweza kuwaletea ili msikwame kwenye utekelezaji wa miradi hii,” amesema Mhe. Kipanga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akiongea katika ziara hiyo amemhakikishia Naibu Waziri Kipanga kuwa wamepokea maelekezo yake na kuahidi kushirikiana kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
“Mheshimiwa Naibu Waziri tumepokea maelekezo yako kama Halmashauri na tunakuahidi kushirikiana bega kwa bega na wasimamizi wa mradi kuhakikisha ujenzi huu unaisha kwa muda uliopangwa,” amesema Munkunda.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo cha VETA Wilaya ya Chemba, msimamizi wa mradi Mhandisi Richard Mwakapeje amesema ujenzi wa chuo hicho umekamilika kwa asilimia 68 na kwamba mpaka sasa mradi umegharimu jumla ya Sh. Milioni 898.