…………………………………………………………………….
Na. Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya dhana ya ushirikishwaji wa jamii kwani ndio imekuwa muarubaini wa kupunguza uhalifu hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Khamis Hamza Chilo (Mb) alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi yaliyopo jijini Dodoma, ambapo amelitaka Jeshi hilo kuendelea kujenga ushirikiano na jamii kwani ubia huo una matokeo chanya katika kuzuia uhalifu.
Akikagua Jengo jipya ambalo ndio Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ( lililokuwa jengo la Duwasa) Naibu Waziri Chilo, ameliahidi kuhakikisha anashirikiana bega kwa bega na Jeshi la Polisi katika kuboresha vitendea kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Jengo hilo linakamilika ili watendaji wake waweze kutekeleza majukumu yao katika mazingira mazuri yatakayo wawezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza na watendaji wa Jeshi hilo, Mhe. Chilo ametoa azigo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa, wanaendelea kudhibiti kikamilifu vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia katika jamii kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kuzuia vitendo hivyo pamoja na kuhakikisha hatua thabiti za kisheria zinachukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya ubakaji na ulawiti.
Aidha, amewataka wananchi kuacha tabia ya kumaliza kesi za udhalilishaji wa kijinsia kinyume na utaratibu badala yake washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa ili wahusika waweze kushughulikiwa kisheria.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri Chilo, amelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini licha ya kuwepo kwa uhaba wa vitendea kazi. Lakini pia ameomba ushirikiano wa karibu ili kutatua kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazo likabili Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, wakati akitoa taarifa ya tathmini ya hali ya Ulinzi na Usalama nchini, amesema hali ya usalama ni shwari kwani uhalifu umepungua kwa asilimia 15.5% japo Kuna changamoto ya kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na uhalifu unaovuka mipaka ambao Jeshi la Polisi bado linaendelea kuyashughulikia kwa kufanya operesheni mbalimbali za kuzuia uhalifu.
IGP Sirro alisema kuwa, Jeshi la Polisi limeweka mikakati mbalimbali ya kupambana na uhalifu wa aina yoyote kwa kuendelea kutoa elimu ya ushirikishwaji wa jamii kwa wananchi pia kuhimiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi pamoja na kuwatumia viongozi wa dini na wanasiasa kuwahubiria wananchi kuepukana na vitendo hivyo vya kihalifu.
Aidha, IGP Sirro amewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya kihalifu na badala yake washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Naye kwa upande wake Kamishna wa Kamisheni ya ushirikishwaji wa Jamii wa Jeshi la Polisi, Kamishna Dkt. Mussa Ali Mussa amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa ushirikiano wake kwa Jeshi la Polisi pamoja na kuahidi kuwa, Jeshi la Polisi litatekeleza maagizo yote kama alivyo elekeza.