*********************************************
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije leo kimeanza kwa kupoteza mbele ya Zambia.
Dakika 45 zilikamilika kwa timu zote kumaliza bila kufungana huku Stars ikionekana kupata nafasi za wazi na kushindwa kuzitumia kupitia kwa nyota Ayoub Lyanga ambaye aliumia kipindi cha pili.
Bao la kwanza kwa Zambia ya Micho ambaye aliwahi kuinoa Yanga zamani lilipachikwa na Collins Sikombe kwa mkwaju wa penalti dakika ya 64.
Penalti hiyo ilipatikana katika harakati za kuokoa ambapo Kapombe Shomari alinawa mpira wakati akiokoa hatari akiwa ndani ya 18 na alionyeshwa kadi ya njano ikiwa ni ya kwanza kwa Stars.
Bao la pili lilifungwa na Emmanuel Chabula dakika ya 80 kwa shuti kali ambalo lilimfanya Aishi Manula asiwe na la kufanya.
Nyota wa Zambia, Sikombe amekuwa mchezaji bora wa mchezo baada ya kufunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao kwenye mchezo wa leo.