Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (wapili kushoto), akimkabidhi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, tuzo ya mshindi wa pili miongoni mwa mabanda bora ya Wizara, Idara na Taasisi za serikali.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango na Msemaji wa Wizara hiyo Bw. Benny Mwaipaja, akionesha moja kati ya tuzo mbili ambazo Wizara imenyakua kwenye maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa (DITF), Dar es Salaam
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango na Msemaji wa Wizara hiyo Bw. Benny Mwaipaja, akionesha tuzo mbili ambazo Wizara imenyakua kwenye maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa (DITF), Dar es Salaam
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny Mwaipaja aliyeshika tuzo, (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania-TANTRADE, Bw. Edwin Rutageruka (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bw. Felix Lyaniva, muda mfupi baada ya Wizara ya Fedha na Mipango kukabidhiwa tuzo mbili za mshindi wa pili wa Banda Bora na Mfumo Bora wa Ukusanyaji Maduhuli ya Serikali (GePG)
Baadhi ya washiriki wa Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakifurahia tuzo mbili ambazo Wizara imepata katika Maonesho hayo.
Baadhi ya washiriki wa Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Taasisi zake, wakifurahia tuzo nne ambazo Banda la Wizara limepata katika Maonesho hayo.
…………………………….
Na Mwandishi wetu, WFM, Dar es Salaam
WIZARA ya Fedha na Mipango, imetwaa tuzo mbili kwa mpigo kwenye Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, yanayofikia kilele Jumamosi Julai 13, 2019.
Katika hafla ya ufungaji rasmi wa maonesho hayo kwenye ukumbi wa Rashid Mfaume Kawawa (Ceremonial dome) , Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alikabidhi tuzo hizo moja baada ya nyingine, kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja.
Akizungumzia tuzo hizo Bw. Mwaipaja alisema moja ni ya mshindi wa pili katika ubunifu wa mfumo wa ukusanyaji maduhuli ya serikali (GePG) ambao umerahisisha mfumo wa malipo kwa wananchi, wakiwemo pia wafanyabiashara, na wawekezaji.
Aidha, Taasisi mbili za Wizara ya Fedha na Mipango, ikiwemo Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), zimetwaa tuzo ya mshindi wa Tatu katika utoaji wa Elimu bora ya Juu na Usimamizi makini wa wataalamu wa Ununuzi na Ugavi.
Maonesho hayo yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere maarufu Sabasaba, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, yamebeba kauli mbiu isemayo “Usindikaji wa Mazao ya Kilimo kwa maendeleo endelevu ya viwanda.”