Mkurugenzi wa kampuni ya maziwa Bora kabisa nchini ya Asas ,Ahmed Salim akiwa na mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela wakimkabidhi zawadi za ubingwa kapteni wa timu ya Mtwivila City (Ifuenga) ligi soka daraja la tatu yanayojulikana kwa jina la Asas Super league 2020/2021
………………………………………………………………………………
NA Fredy Mgunda na Denis Mlowe, Iringa
TIMU soka ya Mtwivila City (Ifuenga United) imefanikiwa kuibuka bingwa wa ligi ya mkoa wa Iringa (Asas Super League) msimu wa 2020/2021 kwa kufanikiwa kuibamiza bila huruma timu ya soka ya Ivambinungu FC mabao 3 – 1 katika mchezo wa fainali uliopigwa katika dimba la Samora.
Katika mchezo huo timu ya Mtwivila City (Ifuenga United) ilikuwa timu ya kwanza kupata goli katika dk ya 48 kipindi cha kwanza kupitia Michael Sadat.
Mchezo huo uliohudhuriwa na na maelfu ya mashabiki wakiongozwa na wakuu wa wilaya ,Richard Kasesela, Asia Abdalah na Jamhuri William mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu, Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada hadi kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo yalikuwa moja bila.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa na kupelekea mchezaji wa timu ya Ivambinungu fc Joseph Chatanda kujifunga goli dakika ya 78 baada ya goli hilo timu ya Ivambinungu fc ikachachamaa na kupata goli dakika ya 83 kupitia kwa mchezaji Stanislaus Msemo lakini mchezaji Michael Sadat kufunga goli la tatu lilomaliza kabisa mchezo huo.
Akizungumza mara baada kushinda ubingwa huo kocha wa timu ya Mtwivila city (Ifuenga United) Edger Nzelu alisema atakikisha timu hiyo inapambana kushinda ligi ya kanda ili kwenda hatua inayofuata.
Alisema kuwa timu hiyo inawachezaji na viongozi ambao wamekuwa wakishirikiana vizuri na ndio faida ya kupata kushinda wa ubingwa huo wa mkoa wa Iringa.
Naye mfadhili wa timu hiyo Joseph Kilienyi alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanashinda ligi ya kanda kwa kuwa timu hiyo imejipanga kisawasawa kuwa mabingwa wa kanda.
Alisema kuwa wanataka kwenda kanda na kuhakikisha timu hiyo inafika katika madaraja ya juu na hatimaye kufika ligi kuu Tanzania bara.
Timu ya mtwivila city (Ifuenga) imejipanga kwa kila kitu hivyo wamekuwa mabingwa wa mkoa watahakikisha timu hiyo hairudi nyuma tena kwenye ligi ya mkoa wa Iringa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni ya maziwa Bora kabisa nchini Ahmed Salim Abri alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa Bora na kuwashukuru chama Cha mpira wa miguu mkoa wa Iringa kwa kufanikisha Hilo.
Alisema kuwa Kama wadhamini wa mashindano hayo mkataba wa miaka mitatu umemalizika Ila kutokana na maombi ya chama hicho analichukua wazo la kuongeza mkataba na IRFA kulifikisha kwa uongozi wa Asas.
Ahmed Salim aliwashukuru wanahabari kwa kuweza kutangaza vyema mashindano hayo na kuipa thamani kampuni ya Asas .
Kwa upande wake mgeni rasmi wa mashindano hayo , Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliishukuru kampuni ya Asas kwa kudhamini na kutoa wito kwao kuongeza mkataba kwani wamefanikisha soka la mkoa wa Iringa kukua kwa kiasi kikubwa kwa kujitoa kwao.
Alisema kuwa kampuni ya maziwa ya Asas imekuwa ikijitoa kwa jamii katika nyanja zote Hali ambayo wadau wengine wanatakiwa kuiga.