Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma Theofanes Mlelwa mwenye shati la kitenge akishiriki ujenzi wa Bweni la wavulana katika shule ya sekondari Wino linalojengwa kwa nguvu za wananchi na kwa kushirikiana na Serikali ambayo imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya viwandani,kushoto mkuu wa shule hiyo Benaya Mkumba.
Picha na Muhidin Amri
……………………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Madaba
KUTOKANA na uhaba mkubwa wa Mabweni unaowakabili wanafunzi wa shule ya Sekondari Wino Halmashauri ya wilaya Madaba,Wananchi kata ya Wino yenye vijiji vitatu vya Wino,Lilondo na Igwisenga wameanza ujenzi wa Bweni moja la wavulana litakalokuwa na uwezo wa kuchukua watoto 80.
Kutokana na uhitaji mkubwa wa mabweni katika shule hiyo wanafunzi hasa wa kiume kwa sasa wanalazimika kupanga vyumba uraini jambo lililochangia sana kushuka kwa taaluma na morali ya kujisomea kwa wanafunzi .
Akizungumza katika eneo la ujenzi Afisa Mtendaji wa wa Serikali ya kijiji cha Wino Sholastika Mkanula amesema, wananchi wamehamasika kujitokeza kuchangia nguvu zao na vitu mbalimbali katika ujenzi wa bweni ili kupunguza tatizo la sehemu ya kulala wanafunzi wa kiume.
Alisema, katika ujenzi wa bweni la wavulana wananchi kupitia mitaa yao kila mmoja amehamasika kwa kuleta mawe,matofali na mchanga kwa ajili ya ujenzi huo .
Hata hivyo,amewaomba wadau wengine wa maendeleo kutoka maeneo mbalimbali kuwaunga mkono kwa kuchangia ujenzi bweni hilo ambalo mara litakapokamilika litachangia sana kurudisha morali ya kujisomea na kupanda taaluma kwa wanafunzi na shule kwa jumla .
Alisema,kitendo cha wananchi wake kujitokeza kushiriki kwa hali na mali ujenzi huo kimemtia moyo na kuhaidi kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Hezron Mwageni amesema,mradi huo ulianza tangu mwezi 8 ambapo wananchi walitakiwa kuchangia nguvu zao kwa kuchimbi msingi,kuleta mawe,matofali na mchanga jambo ambalo wamelitekeleza kwa kiwango kikubwa.
Alisema, wananchi wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuhakikisha watoto wa kiume katika shule hiyo nao wanakuwa na mazingira mazuri na salama ya kuishi na kuwataka wananchi ambao bado hawajachangia wanafanya hivyo ili kuwezesha watoto wao kuishi katika mazingira mazuri na kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa shule hiyo Benaya Mkumba amesema, kwa sasa shule ya Sekondari Wino ina uhitaji wa mabweni 4 kwa ajili ya wavulana na yaliyopo 4 ambayo yanatumika kwa wasichana, kwa hiyo kujengwa kwa bweni hilo kunakwenda kupunguza mahitaji ya mabweni kwa wanafunzi wa kiume .
Alisema, katika ujenzi huo Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya kununua vifaa vya viwandani na mara litakapokamilika litasaidia kuinua taaluma na kujenga nidhamu ya wanafunzi wenyewe hasa ikizingatia kuwa vijana wengi wa kiume wanaishi nje ya eneo la shule.
Alisema, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa sehemu ya kulala, kuna uwezekano mkubwa idadi hiyo itaongezeka na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada za wananchi na serikali kwa jumla.
Naye AfisaMtendaji wa kata ya Wino Hans Pope, ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 80 ambazo zitatumika kununua vifaa vya viwandani, ambapo alisema bweni litakapokamilika litaleta tija kubwa ya kupunguza tatizo la malazi kwa wanafunzi wa kiume.
Amewataka Watanzani, kuhakikisha wanashirikiana na Serikali yao katika ujenzi wa miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo ili kumaliza baadhi ya kero za muda mrefu, badala ya kuichia Serikali kufanya kila jambo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Shafi Mpenda alisema, baadhi ya shule za sekondari ikiwemo Wino zinakabiliwa na upungufu wa mabweni,hata hivyo mkakati uliopo ni kuhakikisha shule zote za sekondari kuna mabweni ya kutosha.
Kwa mujibu wa Mpenda,changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha na kuwaomba wadau mbalimbali wakiwemo wazazi na jamii kwa jumla kujitolea kusaidia katika kuwezesha mpango wa kuimarisha na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifundishia.
Amempongeza diwani wa kata ya Wino na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyoTheofenasi Mlelwa kwa ushiriki na kufuatilia kwa karibu ujenzi wa bweni hilo.