Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Simon Msoka akizungumza na Wasajili Wasaidizi wa NGOs kutoka Halmashauri za Mkoa huo wakati akifungua mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi hao.
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao akitoa maelezo kuhusu majukumu ya Wasajili Wasaidizi katika mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs Mussa Leitura akifafanua jambo kwa Wasajili Wasaidizi katika mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi hao kutoka Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro.
Wasajili Wasaidizi wa NGOs kutoka Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na Ofisi ya Msajili wa NGOs kutoka Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.
…………………………………………………………………..
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Na Mwandishi Wetu, Moshi
Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kuwajibika katika nafasi zao kusaidia usajili na uratibu wa NGOs mkoani humo ili Mashirika hayo yafanye kazi kwa mujibu wa Sheria.
Agizo hilo limetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Msoka alipokuwa akifungua mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi kutoka katika Halmashauri za Mkoa huo.
Msoka amesema Wasajili Wasaidizi wanawajibiķa kuhakikisha NGOs zinafanya Kazi kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ni jambo la umuhimu sana kwani litasaidia uwajibikaji wa Mashirika hayo katika utekelezaji wa Mipango mbalimbali ya Maendeleo.
Ameongeza kuwa ni jukumu la Wasajili Wasaidizi kuhakikisha wanafuatilia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maeneo yao kuwa yanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo.
“Tumepewa dhamana na Serikali katika hili niwaombe muwajibike mfanye kazi kwa moyo wenu na uwezo wenu wote tufanikishe hili lililokusudiwa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo” alisisitiza
Kwa upande wake Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amewataka Wasajili Wasaidizi wa NGOs nchini kuitendea haki nafasi hiyo waliyoteuliwa kwa Mujibu wa Sheria na kuyabeba majukumu yao ili kuyatekeleza kwa ufanisi.
“Sheria imesema Wasajili Wasaidizi watateuliwa Maafisa wa Umma ila tuliona Kada ya Maendeleo ya Jamii inafaa katika kutekeleza jukumu hili la usajili na utaribu wa NGOs katika ngazi za mikoa na Halmashauri” alisema
Akitoa mada katika mafunzo hayo Afisa Ufuatiliaji na Tathmini na Mussa Leitura amesema Wasajili Wasaidizi wanatakiwa kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi yawe yamesajiliwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Akizungumzia kwa niaba ya Wasajili Wasaidizi hao Msajili Msaidizi Mkoa wa Kilimanjaro Hilda Lauwo amemuhakikishia Msajili wa NGOs kusimamia Wasajili Wasaidizi katika Halmashauri ili waweze kutimiza wajibu wao walipewa wa kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maeneo yao.
Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs inaendelea na Mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi katika mikoa na Halmashauri za Wilaya Tanzania Bara kwa lengo la kuwajengea uwezo katika Usajili na Uratibu wa NGOs katika Ngazi za mikoa na Halmashauri.