Meneja wa wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida Mhandisi Masige Matari, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ,Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, wakati Waziri huyo alipotembelea Ujenzi wa Daraja la Sibiti Mkoani Singida.
Muonekano wa sasa wa Daraja la Sibiti ulivyokamilika, lenye upana wa mita 81,ambapo mita 41 zipo katika Mkoa wa Singida na mita nyingine 41 zipo katika mkoa wa simiyu na limegharimu takribani shilingi bilioni 28.
**************************************************
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, ameridhishwa na ujenzi wa daraja la Sibiti linalounganisha mkoa wa Simiyu na Singida.
Waziri Chamuriho ameyasema hayo mkoani Singida wakati alipokagua daraja hilo lililokamilika kujengwa na mkandarasi Hainan International na kuimarisha usafirishaji wa mazao na huduma za usafiri kati ya wilaya ya Meatu na Mkalama.
“Daraja limekamilika hivyo basi naagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kukamilisha ujenzi wa barabara za maungio ya daraja zenye urefu wa kilometa 25, ili daraja liwe imara na usalama zaidi”, alisema Waziri Chamuriho.
Aidha, ameiagiza TANROADS kulitunza daraja hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu.
Awali akitoa taarifa, Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida, Mhandisi Masige Matari, amemueleza Waziri Mhandisi Chamuriho kuwa Daraja hili lina upana wa mita 82, ambapo mita 41 zipo katika mkoa wa Singida na mita nyingine 41 zipo katika mkoa wa Simiyu.
Mhandisi Masige, amefafanua kuwa ujenzi wa daraja na barabara zake za maungio utafungua uchumi wa wananchi wa Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa na pia itapunguza kilometa 200 ambazo zilikuwa zikitumika kutoka Singida hadi Musoma kwa kupitia Nzega, Shinyanga, Mwanza hadi Musoma.
“Ukipita njia ya Nzega, Shinyanga, Mwanza hadi Musoma ni kilometa 720 lakini ukitokea Singida, Simiyu mpaka Musoma ni kilometa 520 hivyo basi barabara hii ni njia fupi kwa wasafiri na wasafirishaji”, amesema Mhandisi Masige.
Vile vile wananchi wanaopita katika Daraja hilo wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Daraja hilo la Sibiti na kufanya usafirishaji uwe wa haraka tofauti na hapo mwanzo, mvua zikinyesha usafiri ulikuwa wa shida sana.
Takriban shilingi bilioni 28 zimetumika katika ujenzi huo.