Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Gasper Balyomi katikati na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hemed Hailu kulia wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa ambapo Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza Halmashauri hiyo kushika nafasi ya kwanza kukusanya mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2019/2020,kushoto Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga vijijini Juma Mnwele.
Picha na Muhidin Amri.
**********************************************
Na Muhidin Amri,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme, ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Tunduru kwa kufanikisha kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 121.87 katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuufanya mkoa huo kushika nafasi ya kwanza kimkoa.
Mkuu wa mkoa amesema hayo jana wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa(RCC)kilichofanyika mjini Songea na kusistiza kuwa,Halmashauri hiyo imeonesha mfano bora katika suala zima la ukusanyaji mapato na kuzitaka Halmashauri nyingine kuongeza jitihada za makusudi ili kufikia malengo iliyopewa.
“nakupongeza sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Gaspar Balyomi,hakika umefanya kazi kubwa na mzuri katika suala zima la kukusanya mapato ya ndani,hongere sana kwa kazi nzuri unapaswa kuigwa na wakurugenzi wengine wa mkoa wangu”alisema.
Alisema, mafanikio hayo yametokana na dhamira ya kweli kwa watumishi wake, kudhibiti upotevu wa fedha zinazokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali na kudhibiti matumizi ya ovyo ambayo yanasababisha baadhi ya Halmashauri kushindwa kufikia malengo yake.
Mkuu wa mkoa, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwani tangu imeanza kutumia stendi kuu ya Shule ya Tanga kuanzia tarehe 1 Januari 2021 imeongeza mapato ya ndani yatokanayo na ushuru wa stendi na choo kutoka shilingi 200,000 hadi kufikia 900,000 kwa siku.
Aidha, amefurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Mamlaka ya mapato(TRA) ambayo kwa mwaka wa fedha 2019 imeweza kukusanya bilioni15,885,857,987.22 sawa na asilimia 94 na katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021 tayari imekusanya jumla ya shilingi bilioni 16,365,091,735.82 ambayo ni sawa na asilimia 105.
Mndeme alisema, kutokana na kazi nzuri zinazofanywa na idara,sekta na taasisi za serikali mkoa unatarajia kuongeza mapato yatokanayo na kodi pamoja na ushuru kwa kuwa barabara ya Ushoroba wa Mtwara imefunguka na kupelekea maeneo kutoa fursa nyingi za kibiashara ambazo zipo katika maeneo mengine ya nchi nan chi jirani za Malawi na Msumbuji.
Alisema, maeneo hayo yanaunganishwa na kuwepo kwa usafiri wa ndege kupitia uwanja wa Songea ambao upo katika hatua za mwisho za kukamilika na utaanza kufanya kazi hivi karibuni sambamba na Meli ya MV Mbeya 11 iliyoanza kazi ya kusafirisha abiria na mizigo kati ya mkoa wa Mbeya na Mbambabay kupitia Ziwa Nyasa.
Akizungumzia hali ya chakula katika msimu wa mavuno 2019 hadi 2021 ambacho chakula chake kinatumika katika msimu wa 2020/2021 alisema, mkoa ulifanikiwa kuvuna tani 1,355,509 wakati mahitaji ya wakazi wa mkoa huo ni tani 469,172 na kuwa na ziada ya tani 886,337.
Alisema, uzalishaji huo unaufanya mkoa wa Ruvuma kuendelea kushika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa mara ya pili mfululizo na hayo ni matokeo ya wananchi wa mkoa huo kwa kuendelea kujituma katika shughuli za kilimo bila kulazimishwa.
Kuhusu ununuzi wa mazao ya ufuta,mbaazi na soya kwa msimu wa kilimo 2020 umefanyika kupitia mfumo wa stakabadhi mazao gharani ambapo umesaidia kupatikana shilingi bilioni 28,715,523,054.50 kati ya hizo,mapato ya ufuta ni shilingi bilioni 25,062,688,275.50,Soya bilioni 1,067,158,147.00 na mbaazi shilingi bilioni 2,585,676,632.00.
Alisema, mkoa unaendelea kushirikiana na taasisi zingine za serikali katika kusimamia zoezi la ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima ambapo hadi sasa jumla ya kilo milioni 14,826,644 za zao hilo zenye thamani ya shilingi bilioni 33,893,774,357.00 zimeuzwa na minada bado inaendelea.