Afisa Kilimo mseto wa radi wa VIUNGO, Waleed Rashid Juma akizungumza na wakulima wa Shehia ya Pembeni Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wa mkutano wa kuutambulisha wa mradi huo kwa wakulima.
Mkulima wa shehia ya Kiungoni Kassim Abdalla Ali akichangia wakati wa mkutano wa kuutambulisha mradi huo kwa wakulima mapema siku ya Jumatatu Januari 11.
Wakulima wa shehia ya Pembeni wakifuatilia maelezo kutoka kwa maafisa wa Mradi wa VIUNGO wakati wa mkutano wa kuutambulisha mradi huo kwa wakulima wa shehia hiyo.
Wakulima wa shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete Pemba, wakifuatilia maelezo kutoka kwa maafisa wa Mradi wa VIUNGO wakati wa mkutano wa kuutambulisha mradi huo kwa wakulima wa shehia hiyo.
……………………………………………………………………………………
PEMBA.
WAKULIMA katika shehia za Kiungoni, Kinyikani, Pandani na Pembeni Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema uwepo wa mradi wa Viungo, Mboga na Matunda katika shehia zao utasaidia kurejesha hamasa ya uzalishaji wa bidhaa za kilimo hicho tofauti na sasa ambapo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa masoko pamoja na miundombinu duni za uzalishaji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano ya kuutambulisha mradi huo kwa wakulima wa shehia hizo walisema mradi huo umekuja katika muda mwafaka ambapo wakulima wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa wanazozizalisha shambani jambo ambalo hupelekea kupata hasara zaidi kuliko faida.
Ali Said Khamis kutoka Shehia ya Kiungoni alisema ujio wa mradi huo utasaidia kubadilisha maisha yao ikiwa ni pamoja na kuongeza hamasa kwa wakulima kuendelea na uzalishaji kwani wengi wao wanashindwa kuendelea na shughuli hizo kutokana na ukosefu wa soko la uhakika pamoja na miundombinu mibovu ya kuwezeha kilimo cha kisasa.
“Kwakweli sisi wakulima tunashukuru sana na tunaupokea mradi huu kwa mikono miwili kwani tunaamini unakuja kutatua kilio chetu cha siku nyingi ambacho ni soko. Tunazalisha sana mazao lakini hatuna sehemu ya kuyauza na kupelekea kuozea majumbani mwetu,” Alisema.
Aidha aliongeza kuwa kwa muda mrefu wakulima wengi Zanzibar wameshindwa kuendelea kiuchumi kutokana na kulima kilimo kisicho na tija hivyo kupelekea wengi wao kukata tamaa na uendelezaji wa shughuli hizo.
“Tegemeo letu wengi ukiachilia mbali kazi za Pwani shughuli nyingine tunayoitegemea sisi wanyonge ni kilimo, lakini kilimo hiki kwa muda mrefu kimeshindwa kutusaidia kutatua matatizo yetu kwenye familia kutokana na hatua miundombinu mizuri ya kuwezesha kilimo chenye manufaa,” aliongeza.
Alibainisha kuwa, “nimelima shamba langu la matikiti na mitungule mpaka sasa yamekomaa na nimeyavuna lakini nimerundika ndani yanaoza tu sina sehemu ya kuuza, bidhaa tunazo lakini pa kuuza hatuna. Hivyo tunaomba sana mradi huu uje utusaidie kutatua changamoto hizi tunaumia sana wakulima.”
Nae Mtumwa Busra Moh’d, alisema wanawake watakuwa msitari wa mbele kuchangamkia fursa hiyo kutokana na mradi huo kuwalenga wanawake zaidi hivyo itawasaidia kukuza vipato vyao.
“Wanawake tunashindwa kujiendeleza kutokana na kukosa pakuanzia, lakini tunakuhakikishia kwa neema hii iliyotujia leo, sisi wawawake wa shehia hii tutakuwa wakwanza kujitokeza kusajiliwa kwani tunataka sana huu mradi,” alisema.
Mapema akitambulisha mradi kwa wakulima hao, afisa kilimo wa mradi, Yahya Khatib Suleiman alisema mradi huo umekuja kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wakulima kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa masoko, uzalishaji kwa wingi wa bidhaa na zenye ubora unao takiwa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko.
“Naomba mtambue kwamba mradi huu ni wa kibiashara na lengo lake kubwa ni kuja kuongeza wingi na ubora wa mazao sokoni kupitia kuwawezesha wakulima kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko kwa kuzingatia mzunguko wa uzalishaji ili kuongeza uchumi shirikishi kwa wakulima wenyewe,” alisema.
Nae afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mradi huo, Asha Mussa Omar, alisema mradi huo umeweka kipaumbele zaidi kwa wanawake na vijana kutokana na changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo katika sekta ya kilimo.
“Mradi huu unalenga kuwafikia asilimia 55 ya wanawake kati ya wote watakaonufaika na mradi huu kwa lengo la kuwaongezea wanawake fursa za kiamaendeleo,” alisema.
Alisema kupitia mradi huo wanawake watawezeshwa mbinu mbalimbali za kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja elimu ya bustani ya nyumbani kwa lengo la kuongeza lishe bora katika familia.
Zoezi la utambulishaji wa mradi huo katika ngazi ya Shehia unaendelea katika hatua za mwisho kwa shehia zote 50 Unguja na Pemba lenye lengo la kuwafanya wakulima kuutambua mradi huo kabla ya zoezi la usajili wa wakulima kuanza.
Mradi wa Viungo, Mboga na Matunda unatekelezwa na taasisi za People’s Development Forum, Community Forests Pemba pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya na kusimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.