NA EMMANUEL MBATILO
Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) limeyatumia mashindano ya Mapinduzi Cup kama jukwaa la kutoa elimu kwa wachezaji na waajiri kuhusu umuhimu wa bima kwa wachezaji kwani wanapokuwa uwanjani ni rahisi kupata majeraha mbalimbali.
Akizungumza katika Mashindano hayo yanayoendelea Visiwani Zanzibar Meneja wa Uhusiano NIC Bw.Karimu Meshack amesema wameamua kutoa elimu kupitia mashindano hayo kwa wachezaji na waajiri kwani wachezaji wengi Wakitanzania hawana bima.
“Wachezaji wengi Wakitanzania kwenye mpira wa miguu hawana bima na mpira wa miguu unahusisha ajari kwa maana ya majeraha mbalimbali wakati mwingine wanapoteza maisha ndani ya viwanja”. Amesema Bw.Meshack.
Aidha Bw.Meshack amesema waajiri na wachezaji kuna umuhimu kwa wo kuwa na bima kitu ambacho kitawasaidia baadae kwani mwajiri anaweza kununua mchezaji mpaka kwa milioni 200 mchezaji mmoja hivyo mchezaji hana garantii anaweza kucheza muda gani bila kupata majanga yoyote.
“Umeshamnunua mchezaji kwa milioni 200 anacheza mechi moja anakuwa nje kwa msimu mzima ile hasara ni nani anaifidia lakini wangelikuwa na bima kutoka Shirika la Bima la Taifa la NIC lingeweza kusaidia”. Amesema Bw.Meshack.
Hata hivyo ikumbukwe kwamba NIC ni mdhamini wa Mapinduzi cup kwa jumla ya sh 14.7 milioni.
Siku ya kesho mashindano hayo yanafikia tamati ambapo fainali itapigwa kati ya Simba na Yanga kumtafuta mbabe wa mashindano hayo kwa mwaka 2021.