Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya Morogoro katika mkutano uliofanyika jana mkoani Morogoro. Picha na Suleiman Msuya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro, Kibena Kingo akifungua mkutano wa siku moja kwa madiwani wa halmashauri hiyo uliondaliwa na TFCG, Mjumita na TaTEDO kujadili namna ya kuendeleza mradi wa Mkaa Endelevu.Picha na Suleiman Msuya.
Madiwani wa Halmashauri ya Morogoro wakiwa kwenye mkutano uliondaliwa na TFCG, Mjumita, TaTEDO kuhusu matokeo ya mradi wa TTCS na namna ya kuendeleza. Picha na Suleiman Msuya.
***************
NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, ameliomba Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania (TaTEDO) kuiweka halmashauri hiyo katika awamu ya tatu ya Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Kingo ametoa ombi hilo jana wakati akifungua mkutano wa madiwani wa halmashauri hiyo uliofanyika mkoani Morogoro kwa kushirikisha madiwani 31 wa kuchaguliwa na 10 wa viti maalum wa wilaya hiyo.
Alisema halmashauri inatambua mchango wa mradi huo kwenye sekta mbalimbali kama elimu, afya, mazingira, maji na miundombinu.
Mwenyekiti huyo aliomba mashirika hayo kuiweka wilaya hiyo kwa mradi wa awamu ya tatu ili waweze kufikia malengo yanayotarajiwa.
“Ni kweli mmesema Novemba mwaka huu mnamaliza mradi sisi madiwani wa Halmashauri ya Morogoro tunaomba muingize halmashauri yetu kwenye awamu ya pili ya mradi tumejipanga kuendeleza,” alisema.
Alisema vijiji vitano ambavyo ni vya Mlilingwa, Diguzi, Matuli na Lulongwe vimepata mafanikio ambayo yanapaswa kuendelezwa.
Diwani huyo wa Ngerengere alisema halmashauri imekubaliana kutumia Msitu wa Sesenga Lumbachini kutekeleza mradi huo hivyo iwapo mradi wa awamu ya tatu utahusisha wilaya yao watafanikiwa zaidi.
Kingo alisema TTCS imechochea uhifadhi, uzuiaji uvunaji haramu na holela na utunzaji mazingira hivyo ni mradi wa kuungwa mkono.
Alisema mradi umesaidia kuondoa wavunaji haramu na kuwa walinzi wa misitu huku wakijihusisha na miradi ya ujasiriamali kama ufugaji wa kuku na hisa.
Mwenyekiti aliwataka madiwani wenzake kufikisha elimu ya mkaa endelevu kwa wananchi wao ili waweze kuendeleza misitu.
Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema wameamua kuwakutanisha madiwani hao ili kuwapa hali halisi ya mradi na waweze kujiandaa kuendeleza wakati mradi unamalizika.
Alisema iwapo madiwani watasimamia na kuendeleza mradi huo vijiji, wananchi na halmashauri watanufaika huku uhifadhi ukiendelea.
Mkurugenzi huyo msaidizi aliwataka madiwani kutumia Sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999 kwa vijiji kusimamia ardhi yake kwa kuendeleza kwa miradi yenye tija.
“Kwa mwaka zaidi ya hekta 469,000 zinapotea sasa njia ya kukabiliana na hali hiyo ni vijiji kwa kushirikiana na halmashauri kupitia Sheria namba 4 na 5 ya mwaka 1999,” alisema.
Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard alisema mradi huo umefanya mapinduzi ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na maendeleo.
Alisema rasilimali misitu ni fursa muhimu kwa vijiji ambavyo vinayo hivyo ni jukumu la viongozi hasa madiwani kuitumia.