Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kuhusiana na shamba la Mikorosho la Mkwese-Masigati wilayani Manyoni mkoa wa Singida akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja tarehe 11 Januari 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Manyoni Rahabu Jackson.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia Korosho zilizovunwa kwenye shamba la Korosho la Mkwese- Masigati wilayani Manyoni mkoa wa Singida akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika mkoa huo tarehe 11 Januari 2021. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni Charles Fussi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitoka katika ghala la kuhifadhia korosho katika shamba la Korosho Mkwese- Masigati wilayani Manyoni mkoa wa Singida akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika mkoa huo tarehe 11 Januari 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni Charles Fussi.
Moja ya mti wa Mkorosho katika shamba la Mkwese- Masigati wilayani Manyoni mkoa wa Singida lililotembelewa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi tarehe 11 Januari 2021.
………………………………………………………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepiga marufuku viongozi wa vijiji na vitongoji katika maeneo mbalimbali nchini kujihusisha na uuazaji ardhi ikiwemo mashamba kwa kuwa hawana mamlaka ya kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya ardhi Vijji ya mwaka 1999.
Akizungumza wakati akikagua shamba la mikorosho la Mkwese-Masigati wilayani Manyoni mkoani Singida tarehe 11 Januari 2021 akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo alisema, viongozi wa wilaya na halmashauri wanapaswa kukomesha tabia hiyo ya baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji kuuza ardhi kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, ugawaji ardhi kwenye vijiji lazima ufuate sheria iliyowekwa ikiwemo kuitisha mkutano na siyo kiongozi kujiamulia kugawa ardhi kwa niaba ya kijiji kizima.
“Kijiji kugawa ardhi lazima iwe kwenye mutano siyo mtu anagawa, Mkuu wa Wilaya pita kote na elekeza mikutano ya kugawa ardhi isiitishwe kinyemela na wewe ukasimamie kujua wananchi watapata faida gani kwa ardhi itakayotolewa” alisema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kuwa, mtu yoyote atakayenunua ardhi kwa mwenyekiti wa Kijiji au kitongoji basi ajue kuwa ni kinyume cha sheria kwa kuwa ardhi inatakiwa kuamuliwa katika mkutano.
Lukuvi aliipongeza halmashauri ya wilaya ya Manyoni kwa uamuzi wa kugawa mashamba kwa ajili ya kilimo cha korosho na kueleza kuwa uamuzi huo unaifanya Manyoni kusonga mbele na kushauri kupewa muda ili kuona matokeo.
Aliitaka halmashauri ya Manyoni katika mkoa wa Singida kuhakikisha eneo hilo la shamba la Mikorosho linapangwa kimji kwa kubuni mpango wa maendeleo na kufurahishwa na uamuzi wa halmashauri hiyo kuwa na mpango wa kumilikisha ekari 22,000 na kusisitiza kuwa, wote watakaomilikishwa lazima wapatiwe hati za ardhi.