Mratibu wa Lishe kutoka Tamisemi Mwita Waibe akisistiza jambo wakati wa semina hiyo |
MSHIRIKI kutoka wilaya ya Kyerwa akiomba Shirika la Agri Thamani liandae vitini kwa ajili yao ili waingie field maana hawana muda wa kupoteza hii ni ajenda kuu |
VIONGOZI wa Wanawake (UWT) kutoka wilaya za Kyerwa ,Ngara ,Karagwe na Missenyi wakifuatilia semina hiyo
Viongozi wanawake wakifuatilia semina hiyo
MPANGO Jumuishi wa Lishe wa Taifa wa Mwaka 2016-2021 unatambua Viongozi wa Kisiasa kama Wadau Muhimu katika kuimarisha Lishe Bora na kutokomeza udumavu na aina zote za utapiamlo nchini Tanzania.
Kulingana na utambuzi huo, Agri Thamani imeendelea na mpango unaolenga kuwajengea uelewa wa kina Viongozi wa Kisiasa ili waweze kutumia ushawishi wao kwenye jamii kuchangia kubadilisha mfumo mzima wa mahusiano yetu na chakula na pia waweze kufuatilia, kutathmini na kusimamia utekelezaji wa mipango mizuri inayowekwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa UWT wilaya nne za Mkoa wa Kagera ,Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani Neema Lugangira (MB) amesema katika jitihada za kuhakikisha kuwa mkoa huo unatokomeza Udumavu maana ndio Mkoa unaongoza kwa Idadi Kubwa Zaidi ya Watoto chini ya Umri wa Miaka 5 wenye Udumavu;
Alisema Shirika hilo lilianzisha Programu ya kuwafikia Viongozi wa Jumuiya ya Umoja Wanawake Tanzania (CCM) ili kuwajengea uwezo kwa lengo la kupata uelewa juu ya umuhimu wa lishe bora na hatimaye kuweza kuwa chachu ya kutokomeza udumavu kwenye maeneo yao.
“Kama mnavyojua Makao Makuu ya Agri Thamani yapo kwenye Majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera hivyo ni muhimu kwa Agri Thamani kuweka mikakati thabiti na endelevu ili Mkoa wa Kagera uwe Mkoa wa Mfano katika Vita Dhidi ya Udumavu na Utapiamlo kwa Ujumla”, alisema Mhe Neema Lugangira (Mb) – Mkurugenzi wa Agri Thamani.
Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi cha mwezi Desemba 2020 hadi Januari 2021 Agri Thamani ilishatoa Semina za Lishe Viongozi wa UWT kutoka Kata zote za Wilaya za Muleba, Bukoba Mjini na Bukoba Vijijini. Pia, Agri Thamani imeshatoa Semina ya Lishe kwa Madiwani wa Viti Maalumu kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Kagera.
Alisema kwa sasa Shirika hilo la Agri Thamani limekamilisha Mafunzo ya Lishe kwa Awamu ya kwanza kwa kuwafikia Viongozi wa UWT kutoka Kata zote za Wilaya za Ngara, Kyerwa, Karagwe na Missenyi.
Mafunzo haya yalitolewa na Mbunge Neema Lugangira na Mratibu wa Lishe kutoka TAMISEMI, Ndg. Mwita Waibe.
Hata hivyo Viongozi hao wa UWT walionekana kushtushwa na hali ya lishe kwenye Mkoa na maeneo yao kwa namna ambavyo watoto wanaweza kupata athari pasipo mzazi kujua kumbe ambazo zinasababishwa na masuala ya kilishe.
Kwa umoja wao waliazimia kuwa wanakwenda kuhoji kuhusu hali ya lishe kwenye Kata zao, mikataba ya lishe iliyosainiwa kwenye kata zao, bajeti za lishe zinazotengwa na Halmashauri zao na pia ajenda ya lishe inakwenda kuwa ya kudumu kwenye shughuli zao.
Pia Waliaidi kuanza kutoa mafunzo kwa jamii na wameiomba Agri Thamani iandae mafunzo ya vitendo hususan kwenye eneo la namna bora ya kuandaa na kupika chakula chenye lishe bora kwa mama mjamzito, mama anaenyonyesha na mtoto chini ya umri wa miaka 5.
Katika Awamu ya Pili ya Mafunzo haya, Agri Thamani inatarajia kuwafikia Viongozi wa UWT na Madiwani kutoka Mikoa ya Kigoma, Tanga, Tabora, Lindi na Geita kwa Wilaya zitakazochaguliwa. Aidha, chini ya Programu hii hatua inayofuata ni kuwafikia Wenyeviti wa Serikali za Mitaa/Vijiji/Vitongoji, Watendaji wa Kata, na Viongozi wengine Ngazi ya Kata, Kijiji, Kitongoji na Jamii kwa jumla.
Mbunge Neema Lugangira alimalizia kwa kusema wadau wote tukishikiriana kwa karibu na kila mmoja kwa nafasi yake akaibeba Ajenda ya Lishe vita dhidi ya kutokomeza udumavu na utapiamlo tutaishinda ndani ya miaka mitano hii 2020-2025