**************************************************
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka wakazi wa mikoa ya Songwe, Rukwa, Katavi na Kigoma kutumia fursa za ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya barabara na bandari katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ili kukuza uchumi katika maeneo yao.
Amesema hayo leo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za Mpanda-Vikonge (km 35), Kasinde – Mpanda (km 105.389), Kagwira – Karema (km 112) na bandari ya Karema mkoani Katavi ambayo ujenzi wake unaendelea.
Amezitaja fursa hizo kuwa ni kupata ajira kwa wale wenye taaluma, kuzalisha mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na biashara katika mwambao wa ziwa Tanganyika ambao umeanza kuvutia wawekezaji wengi katika siku za hivi karibuni.
“Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 47 za kitanzania kwa ajili ya kujenga bandari ya kisasa ya Karema awamu ya kwanza na mchakato wa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kagwira – Karema (km 112) inayoelekea katika bandari hiyo utaanza hivi karibuni”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.
Amezitaja bandari nyingine zinazojengwa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika kuwa ni Kabwe na Kasanga ambazo zote zitakapokamilika zitaongeza huduma za usafiri na uchukuzi katika Ziwa Tanganyika na nchi jirani hivyo kukuza biashara katika mwambao huo.
Aidha, amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi, kuhakikisha barabara ya Kagwira -Karema (km 112) inayounganisha mji wa Mpanda na bandari ya Karema inapitika wakati wote ili kuharakisha ujenzi wa bandari hiyo na hivyo kuwezesha wawekezaji kufika kwa urahisi katika eneo hilo ili kuona fursa za kiuchumi na kijamii.
Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende, amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.2 za kitanzania zimetengwa kwaajili ya kuiboresha barabara hiyo kipindi hiki cha mvua nyingi wakati mchakato wa kuijenga kwa kiwango cha lami ukiendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando, amesema kuwa Wilaya yake imejidhatiti kuhakikisha wakandarasi wote wanaosimamia miradi katika eneo hilo wanapata ushirikiano wa kutosha ikiwemo ulinzi na watumishi wenye sifa ili kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati.
Bandari ya Karema ambayo inatarajiwa kuwa kubwa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika inajengwa na mkandarasi XIAMEN ONGOING CONSTRUCTION GROUP toka China na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Kukamilika kwa bandari hiyo iliyoko wilayani Tanganyika mkoani Katavi kutachochea biashara kati ya Tanzania na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Burundi na hivyo kukuza uchumi katika mikoa ya ukanda wa magharibi.