Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mkuu wa kitengo
cha Utafiti na Mfunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo
akiwafundisha watoto na watu wazima madhara ya mafuta katika mishipa ya
damu ya moyo wakati wa maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya Dar es
Salaam yanayofanyika jijini Dar es Salaam. Katika maonyesho hayo Taasisi hiyo
inatoa bila malipo ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Alexander Mrosso akimpima mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi (Echocardiography) wakati wa maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya
Dar es Salaam yanayofanyika jijini Dar es Salaam. Katika maonyesho hayo
Taasisi hiyo inatoa huduma za ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo bila
malipo kwa wananchi wanaotembelea banda hilo lililopo ndani ya banda la
Jakaya Kikwete.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakitoa huduma kwa wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa
maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam yanayofanyika jijini
Dar es Salaam. Katika maonyesho hayo Taasisi hiyo inatoa bila malipo huduma
za ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo kwa wananchi wanaotembelea
banda hilo lililopo katika banda la Jakaya Kikwete.
**************
Na Mwandishi Maalum
12/7/2019 Wananchi 1776 wamepata huduma za ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo bila malipo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwenye maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam yanayofanyika katika uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa.
Wananchi hao waliotembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima afya zao walifanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo ambapo 448 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography), na 1097 walifanyiwa kipimo cha kuangalia umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram – ECG).
Asilimia 60 ya watu waliofanyiwa vipimo walikutwa na uzito mkubwa, asilimia 40 walikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na asilimia 20 walikutwa na tatizo la kuwa na sukari kwenye damu.
Aidha Taasisi hiyo hadi sasa imetoa rufaa ya moja kwa moja kwa watu 73 wakiwemo watoto 2 ambao baada ya kuwafanyia vipimo walikutwa na matatizo ya moyo yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina na matibabu ya kibingwa .
Akizungumzia mara baada ya kupata huduma ya matibabu katika banda hilo mkazi wa Shekilango jijini Dar es Salaam Rehema Abdalah aliipongeza Taasisi hiyo kwa kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi bila malipo pamoja na kuwapa kipaumbele wazee waliojitokeza kwenda kupima afya zao.
“Nawashukuru wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wanaotoa huduma katika maonesho haya, kutokana na umri wangu wamenipa kipaumbele cha kufanyiwa vipimo kwa haraka. Nimekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na tayari nimepatiwa dawa kwa ajili ya matibabu,” alishukuru Rehema.
Naye mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam Hatibu Rashid ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafikiria wananchi wenye uwezo wa chini kupata nafasi ya kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo na wafanyakazi wa Taasisi hiyo pindi watakapopata nafasi watoe huduma kama hiyo kwa wananchi waliopo maeneo mbalimbali hapa nchini hasa vijijini.
Rashid alisema, “Zamani vipimo kama hivi vilikuwa vinafanyika nje ya nchi tena kwa watu wenye hela. Lakini leo hii vipimo hivi vinafanyika hapa nchini na tunafanyiwa wananchi wa kawaida kabisa. Ninaishukuru sana Serikali kwa kuimarisha huduma ya matibabu ya moyo na ninawaomba wananchi wenzangu watumie maonesho haya kufika katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupima afya zao bila malipo”,.
Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa bila malipo huduma za ushauri wa lishe bora kwa afya ya moyo, umuhimu wa kufanya mazoezi, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo.