Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu akizungumza na Wasajili Wasaidizi kutoka Halmashauri na Wilaya za Mkoa wa Arusha.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Arusha na Msajili Msadizi wa NGOs wa Mkoa huo Blandina Nkini akizungumzia majukumu ya usajili na Uaratibu wa NGOs wakati wa mafunzo kwa wasanii wasaidizi wa NGOs.
Afisa Ufuatiliaji na tathmini Mussa Leitura akieleza lengo la mafunzo kwa Wasajili wasaidizi wa Halmashauri za Mkoa wa Arusha yanayofanyika mkoani Mkoani hapo.
Wasajili wasaidizi wa NGOs kutoka Halmashauri za Mkoa wa Arusha wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kuhusu Usajili na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ametaka uwajibikaji, uzalendo na maadili ya utumishi wa umma kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri na Mikoa ambao kisheria ni Wasajili wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wanaosimamia Usajili na uratibu wa Mashirika hayo kwa ngazi ya Halmashauri na Mkoa.
Dkt. Jingu ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Mkoa wa Arusha yenye lengo la kuwajengea uwezo na uelewa wa namna bora ya kusajili na kuratibu Mashirika katika ngazi za mikoa na Halmashauri.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa Wasajili wasaidizi hao wanatambulika kisheria hivyo wanatakwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa wakizingatia kuwa wamebeba dhamana kubwa ya kumsaidia Msajili wa NGOs kutambua na kuhakiki Mashirika hayo kabla ya kusajiliwa.
“Tuhakikishe tumatimiza wajibu wetu. Tumechaguliwa kuifanya hii kazi basi tuwe waadilifu, wazalendo na tuzingatie maadili ya utumishi wa Umma katika kuyatekeleza majukumu yetu.” alisema.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa uwepo wa Wasajili Wasaidizi wa NGOs katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri inasaidia Serikali kutambua Mashirika yanayotekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutatua changamoto na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Msajili wa NGOs, Mussa Leitura amewasihi Wasajili wasaidizi hao kumsaidia Msajili wa NGOs katika Usajili na Uratibu wa Mashirika hayo kwa ngazi walizopo.
Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Arusha Blandina Nkini amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kumsaidia Msajili wa NGOs katika hatua za awali za usajili na uratibu wa Mashirika hayo katika utekelzaji wa miradi.