*********************************************
NA SULEIMAN MSUYA
OFISA Sera na Majadiliano wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Elida Fundi amesema iwapo vijiji vyenye misitu ya asili vitatumia rasilimali hiyo kwa njia endelevu vitapata maendeleo kwa haraka.
Fundi amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mtawatawa na Darajani wilayani Liwale mkoani Lindi ambapo alitembelea akiambatana na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.
Amesema misitu ni bidhaa ambayo ina fursa nyingi kama wanavijiji watapata elimu kuhusu faida zilizopo hasa wanapotumia kwa njia endelevu.
Ofisa huyo amesema MJUMITA kwa kushirikiana na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) wamekuwa wakiibua miradi mbalimbali ambayo inasaidia wanavijiji kuona fursa zilizopo kwenye misitu na mwitikio ni mzuri.
“MJUMITA na TFCG tunatambua fursa zilizopo kwenye misitu ndio maana kila kukicha tunabuni miradi kama Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS) ambao umefikia vijiji zaidi ya 30 katika wilaya ya Kilosa, Mvomero na Morogoro mkoani Morogoro.
Pia kwa sasa tunatekeleza Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endeley ya Misitu (CoFoREST) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) imeonesha matokeo chanya ya kimaendeleo, uchumi na jamii,” amesema.
Fundi amesema vijiji venye kutekeleza Mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USMJ) umechochea maendeleo na kuongeza uhifadhi.
Amesema vijiji vimeweza kutekeleza miradi mikubwa kwa muda mchache tofauti na awali ambapo miradi mingi imekuwa ikisuasua.
Ofisa huyo amevitaka vijiji vingine vyenye misitu ya asili kuitumia kwa dhana ya USMJ ili kuweza kuchochea maendeleo yao na ya vijiji.
“USMJ imepunguza mzigo mkubwa kwani misitu imesaidia kutekelezwa kwa miradi ya shule, zahanati, maji, elimu, afya na mingine mingi huku uhifadhi ukiongezeka,” amesema.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Liwale Rajabu Kambangwa amesema wilaya hiyo inatambua mchango wa sekta ya misitu hivyo wataendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa mashirika kama MJUMITA, TFCG na mengine.
Kambangwa amesema misitu ni moja ya chanzo cha uhakika cha mapato wilayani ambapo kwa mwaka wanakusanya zaidi ya shilingi bilioni 2 zinaoelekezwa kwa miradi ya maendeleo.
“Sisi tunakusanya kodi kupitia vyanzo mbalimbali lakini kusema ukweli sekta ya misitu imekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo,” amesema
DAS huyo amesema wamekuwa wakisisitiza wanavijiji kutunza mazingira ili kuhakikisha wanaweza kukabiliana na mabadili ya tabia nchi.
Amesema wanaendelea na utoaji elimu kwa wananchi wa vijiji vyote ambavyo rasilimali mksutuninakuwa rasmi.
Katibu Tawala huyo amesema ushirikiano ndio mbinu pekeee ambayo inaweza kuchochea maendeleo hivyo kuyataka mashirika mengine kujitokeza na kuwekeza kwenye sekta hiyo muhimu.
Amewataka wananchi wa wilaya ya Liwale ambao vijiji vyao vina Vasili misitu ya asili kuitumia vizuri ili kuweza kuondoa changamoto za uhaba wa madarasa, nyumba za walimu, vituo vya afya na huduma nyingine muhimu.
Baadhi ya mwananchi wa vijiji vya Mtawatawa na Darajani wamesema fursa wanazozipata kupitia USMJ ni nyingi hivyo kuahidi kuungamkono miradi ya MJUMITA na TFCG.