Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira. 
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Haruni Mapesa.
………….
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira, amewataka wahitimu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) kutumia maarifa waliyoyapata chuoni hapo kuzingatia maadili na uzalendo katika utendaji wao na kuleta manufaa kwa jamii na Taifa.
Wasira, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho kilichopo Kivukoni, Dar es Salaam, ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mahafali ya 21 ya chuo hicho yaliyofanyika Novemba 20, 2026, yaliyohudhuriwa na wahitimu 4,747, wakiwemo wanawake 2,504 sawa na asilimia 53 na wanaume 2,243 sawa na asilimia 47.
Amesema maadili na uzalendo ni mambo muhimu katika ujenzi wa Taifa na utekelezaji wa majukumu katika sekta ya umma na binafsi, hivyo wahitimu wanapaswa kuyaonesha kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi na katika jamii.
Kwa mujibu wa Wasira, baadhi ya wahitimu wametunukiwa Shahada za Uongozi, Maadili na Utawala, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanatumia elimu waliyoipata kuonesha mfano wa uongozi unaozingatia misingi ya maadili na uzalendo.
Amewahimiza wahitimu hao kwenda kuonesha kwa vitendo ubora wa mafunzo waliyopata katika chuo hicho kwa kutumia ujuzi na maarifa yao kuchochea maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Aidha, ameitambua na kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake katika maendeleo ya chuo hicho, ikiwemo fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza miundombinu.
Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Haruni Mapesa, amesema chuo kimeendelea kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika kampasi zake za Kivukoni, Dar es Salaam na Pemba, sambamba na kuongeza programu za mafunzo ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa.
Amesema katika kampasi ya Kivukoni, chuo kimekamilisha jengo la utawala lenye uwezo wa kuchukua wafanyakazi 70 pamoja na madarasa yanayoweza kuhudumia wanafunzi zaidi ya 500 kwa wakati mmoja, huku kikiendelea na ujenzi wa jengo jingine la mihadhara litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 250.
Profesa Mapesa amesema pia chuo kinaendelea na ujenzi wa mabweni yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500, huku katika kampasi ya Pemba kikikamilisha ukumbi mkubwa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,500.
Amesema uwekezaji huo unatekelezwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imeendelea kuweka fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu na kuongeza uwezo wa chuo kutekeleza majukumu yake.
Katika hatua nyingine, amesema idadi ya programu za mafunzo imeongezeka hadi kufikia 56 katika ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo astashahada, stashahada, shahada ya kwanza na shahada za uzamili, huku chuo kikiendelea kuandaa mitaala kwa ajili ya kuanzisha programu za shahada za uzamivu (PhD).
Kuhusu ongezeko la wanafunzi, Profesa Mapesa amesema idadi ya wanafunzi waliosajiliwa imeongezeka kutoka 1,297 mwaka 2025 hadi kufikia 13,290 mwaka 2026, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wanafunzi na jamii kwa ujumla katika huduma za elimu zinazotolewa na chuo hicho.
Amesema katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 4,747 wanatunukiwa vyeti na shahada katika ngazi mbalimbali, ambapo wanawake ni 2,504 sawa na asilimia 53, huku wanaume wakiwa 2,243 sawa na asilimia 47. Kati ya wahitimu hao, 33 wanatunukiwa shahada za umahiri katika fani mbalimbali zikiwemo uongozi, utawala, rasilimali watu, jinsia na maendeleo.
Ameongeza kuwa chuo kimeendelea kuwekeza katika kuwaendeleza watumishi wake, hususan wahadhiri na wataalamu, kwa kuongeza idadi ya wenye shahada za uzamili na kupandisha vyeo watumishi wa kada ya taaluma, hatua inayolenga kuimarisha ubora wa ufundishaji, utafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalamu.
Hata hivyo, Profesa Mapesa amesema pamoja na mafanikio hayo, chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa baadhi ya nyenzo za kufundishia na kujifunzia, hivyo kinaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kutafuta suluhisho ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilianzishwa kwa lengo la kuendeleza mafunzo ya uongozi na itikadi, kikihusishwa na historia ya Chama cha TANU na mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mwaka 2005 kilibadilishwa jina na kuitwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa lengo la kuenzi mchango wake katika ujenzi wa taifa.

