Meneja wa kampuni hiyo, Owais Yusuf akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam.
………….
Happy Lazaro, Dar es Salaam.
Dar es Saalam .KAMPUNI ya Royal Gems &Jewellery inayojihusisha na biashara ya dhahabu na vito vya thamani, imesema inaendelea kuongeza thamani ya madini yanayopatikana nchini kwa kuyachakata na kuyatengeneza katika mapambo mbalimbali yanayoweza kushindana katika soko la kimataifa.
Akizungumza katika maonyesho ya madini, Meneja wa kampuni hiyo, Owais Yusuf amesema kampuni inajihusisha na utengenezaji wa vito mbalimbali kwa kutumia madini yanayopatikana Tanzania, ikiwemo Tanzanite, dhahabu na almasi kutoka maeneo tofauti kama Mererani, Mahenge na Tunduru.
Amesema tofauti na biashara ya kuuza madini yakiwa ghafi, kampuni hiyo imejikita katika kuongeza thamani ya madini kwa kuyatengeneza kuwa mapambo mbalimbali, hatua inayosaidia kuonesha uzuri na ubora wa madini ya Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.
Owais amesema kampuni pia inapokea oda maalumu kutoka kwa wateja wanaohitaji mapambo yenye michoro au miundo wanayoitaka, ambapo mafundi wenye ujuzi hutumia teknolojia na utaalamu wao kutengeneza bidhaa kulingana na mahitaji ya mteja.
“Ubora wa kazi zinazofanywa na mafundi hao unalenga kufikia viwango vya kimataifa, huku kampuni ikijivunia kutumia rasilimali za ndani na kuonesha uwezo wa Watanzania katika sekta ya uchakataji na utengenezaji wa vito vya thamani.”amesema Owais.
Amefafanua kuwa kampuni hiyo pia inachangia katika kukuza ajira kwa vijana wa Kitanzania kwa kuajiri mafundi pamoja na kutoa nafasi kwa wanafunzi na vijana wanaotaka kujifunza ujuzi wa uchakataji na utengenezaji wa madini kupitia mafunzo kwa vitendo.
Amesema kwa sasa kampuni ina takribani maduka 15 na imeajiri pamoja na kutoa mafunzo kwa zaidi ya vijana 100, wakiwemo wanawake, huku shughuli zake zikiendelea kupanuka katika maeneo mbalimbali nchini.
Owais amefafanua biashara hiyo ina historia ya zaidi ya miaka 20 nchini Tanzania, huku uzoefu wa familia katika shughuli za madini ukifikia vizazi zaidi ya 12.
Kampuni inaendesha shughuli zake katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza na Zanzibar kupitia matawi na majina mbalimbali ya kibiashara kulingana na soko la eneo husika.
