Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR), unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais nchini, Dkt. Damas Mapunda akizungumza katika kikao kilichowakutanisha waratibu na viongozi mbalimbali kutoka halmashauri zinazotekeleza mradi huo cha Kufanya mapitio ya utekelezaji wa mradi, kilichofanyika Mbeya, Novemba 20, 2026.
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR), unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais nchini, Dkt. Damas Mapunda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na waratibu na viongozi mbalimbali kutoka halmashauri zinazotekeleza mradi huo mara baada ya kikao kilichofanyika Mbeya, Novemba 20, 2026.
Baadhi ya waratibu na viongozi mbalimbali kutoka halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) wakiwa katika kikao cha Kufanya mapitio ya utekelezaji wa mradi huo, kinachoendelea mkoani Mbeya Novemba 20, 2026.
Mratibu wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR), Mkoa wa Mbeya Bw. Richard Ngoda akizungumza katika kikao kilichowakutanisha waratibu na viongozi mbalimbali kutoka halmashauri zinazotekeleza mradi huo, kilichofanyika Mbeya Novemba 20, 2026.
…………..
*HABARI*
Wataalamu kutoka sekta mbalimbali wamekutana jijini Mbeya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai Tanzania (SLR), unaolenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kurejesha ardhi iliyoharibika na kulinda bioanuai nchini.
Mradi huo unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi huo Dkt. Damas Mapunda amesema kikao hicho kilikuwa cha siku tano ambacho kimemalizika leo Novemba 20, 2026 jijini Mbeya kilichowakutanisha waratibu na viongozi mbalimbali kutoka halmashauri zinazotekeleza mradi huo ili Kufanya mapitio ya utekelezaji wa mradi.
Amesema Mkutano huo umetoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa mradi, kubadilishana uzoefu na maarifa ya kitaalamu, pamoja na kutathmini hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Amesema Mradi wa SLR unalenga kuimarisha usimamizi jumuishi wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi na misitu iliyoharibika, sambamba na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, mradi huo unalenga kuwawezesha wananchi kutumia rasilimali za mazingira kwa njia endelevu kupitia shughuli mbadala za kiuchumi, zikiwemo kilimo rafiki kwa mazingira, ufugaji endelevu, upandaji miti na shughuli za kuongeza thamani ya mazao.
Naye, Afisa Maliasili na Mazingira Mkoa wa Iringa, Dkt. Guliama Bahati amesema Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri saba ambazo ni Mbeya, Mbarali, Iringa, Wanging’ombe, Sumbawanga, Mpimbwe na Tanganyika, katika maeneo ya Bonde la Ruaha Mkuu na Bonde la Ziwa Rukwa.
Amesema mradi umechangia kuboresha hali ya mazingira, kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na kuhakikisha rasilimali za asili zinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa B. Swaumu Kweka amesema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na uratibu katika utekelezaji wa shughuli za mradi, ili kuhakikisha agenda ya uhifadhi wa mazingira inaenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
