Wamiliki na viongozi wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kuboresha mazingira ya kazi na kulinda maslahi ya Waandishi wa Habari, kwa kuwa usalama wa ajira, malipo ya haki na upatikanaji wa stahiki zao vina mchango mkubwa katika kuboresha ubora na uaminifu wa habari zinazowafikia wananchi.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 20, 2026, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), uliofanyika katika Ukumbi wa Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam.

Wakili Kipangula amesema mwandishi wa habari anayefanya kazi katika mazingira bora ana nafasi kubwa ya kutekeleza majukumu yake kwa uhuru, weledi na uadilifu, hivyo kulinda maslahi ya wafanyakazi ni sehemu muhimu ya kujenga sekta ya habari yenye ubora na inayoaminika.

Amesema maendeleo ya sekta ya habari hayawezi kupimwa kwa idadi ya vyombo vya habari pekee, bali pia kwa namna wafanyakazi wake wanavyothaminiwa, kulindwa na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Aidha, amekihimiza Chama cha JOWUTA kuwa daraja la mazungumzo na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa sekta ya habari, kwa kusimamia maslahi ya wanachama wake kupitia sheria na mazungumzo yenye tija.

Ameeleza kuwa JAB ipo tayari kushirikiana na JOWUTA katika maeneo mbalimbali, yakiwemo kutoa mafunzo endelevu, kuhamasisha uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya habari na kujenga uelewa kuhusu haki na wajibu wa Waandishi wa Habari, kwa kuzingatia mipaka ya kisheria na majukumu ya kila taasisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Bw. Musa Juma Siwayombe, amesema chama hicho kinalenga kuhakikisha wafanyakazi wa vyombo vya habari wanapata mazingira rafiki na salama ya kazi, mikataba halali ya ajira na stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Ameiomba Serikali kuendelea kuimarisha usalama wa Waandishi wa Habari wanapotekeleza majukumu yao, huku vyombo vya dola vikitambua nafasi yao kama wadau muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Mkutano huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Mshikamano, Haki na Maslahi Bora kwa Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari.”