Meneja manunuzi wa kampuni hiyo,Ally Mzee akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Naasir Hussein akizungumza kwenye maonesho hayo jijini Dar es Salaam. 
Afisa manunuzi wa kampuni hiyo, Naila Haydar akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo jijini Dar es Saalam.
………….
Happy Lazaro, Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM. Kampuni ya Sab Gold Limited (SGL) imewawezesha vijana na wachimbaji wadogo kujikwamua kiuchumi kupitia utoaji wa mitaji ya uchimbaji, huduma za usafishaji wa dhahabu na upatikanaji wa masoko, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wao katika sekta ya madini.
Akizungumza katika maonesho ya madini yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Naasir Hussein, amesema kampuni imejikita katika kuwasaidia wachimbaji wadogo, hususan vijana wasiokuwa na mitaji ya kutosha lakini wenye nia ya kujiajiri kupitia shughuli za uchimbaji wa dhahabu.
Amesema kampuni hiyo pia inamiliki kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichopo Kahama na inafanya kazi na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kama wakala wa kuhifadhi dhahabu, huku ikiendelea kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia sekta hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Manunuzi wa kampuni hiyo, Naila Haydar, amesema uwezeshaji unaotolewa na kampuni hiyo umesaidia vijana waliokosa ajira rasmi kujiajiri kupitia uchimbaji wa madini, wakiwemo wanawake ambao wameweza kupata dhahabu na kipato cha kuendesha maisha yao.
Amesema mpango huo unalenga kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwapa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji badala ya kusubiri kuajiriwa.
Naye Meneja manunuzi wa kampuni hiyo,Ally Mzee, amesema kampuni hiyo inashiriki katika ununuzi wa dhahabu na ina kiwanda cha kusafisha madini hayo kilichopo Kahama, hatua inayosaidia kuwaunganisha wachimbaji na huduma za soko.
Amesema uwepo wa kampuni hiyo katika sekta ya madini unalenga kurahisisha shughuli za wachimbaji wadogo kwa kuwawezesha kupata huduma zinazohusiana na biashara ya dhahabu, ikiwemo usafishaji na ununuzi wa madini hayo.
Ally amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kwa kujiunga na shughuli za uchimbaji na kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Wakizungumza namna walivyonufaika na kampuni hiyo ,Mchimbaji mdogo wa dhahabu, Mboje Maziba, amesema kampuni hiyo ya Sab Gold imemsaidia kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zake za uchimbaji, tofauti na awali ambapo walitegemea fedha zao wenyewe na wakati mwingine shughuli kusimama kutokana na ukosefu wa mitaji.
Amesema huduma za kusafisha na kuuza dhahabu zinazopatikana Kahama zimewapunguzia wachimbaji gharama na usumbufu wa kusafiri hadi Mwanza kufuata huduma hizo, huku akiwataka vijana kuwa na bidii na uaminifu katika shughuli za uchimbaji.
Naye Mchimbaji mdogo, Vaileth Shelembi amesema kuingia katika sekta ya madini kumemfungulia fursa za kujipatia kipato na kuboresha hali yake ya kiuchumi, licha ya kuanza shughuli hizo mwanzoni mwa mwaka huu.
Amesema kupitia maonesho hayo amepata nafasi ya kukutana na wachimbaji wakubwa pamoja na wafanyabiashara wa vifaa vya uchimbaji na kujifunza mambo mbalimbali yatakayomsaidia kukuza shughuli zake, huku akiwahimiza vijana wengine kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini.
