Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Baraka Luvanda akizungumza na waandishi mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji katika Wizara hiyo, Jane Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
Happy Lazaro, Arusha.
ARUSHA. Wadau wa mfumo wa haki jinai nchini wametakiwa kuimarisha ujuzi wao wa kitaaluma ili kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu zinazojitokeza kutokana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Baraka Luvanda, wakati wa kufungua mafunzo ya siku tatu yanayowakutanisha wataalamu wanaohusika na upelelezi, uchunguzi na uendeshaji wa mashauri ya jinai jijini Arusha.
Luvanda amesema mabadiliko ya kijamii na kiteknolojia yameifanya sekta ya haki jinai kukabiliwa na mazingira mapya ya kiutendaji, hivyo watendaji wake wanapaswa kuwa na uwezo wa kutambua na kutumia mbinu zinazolingana na aina ya makosa yanayojitokeza kwa sasa.
Amesema mapungufu yaliyobainishwa na Tume ya Haki Jinai iliyoanzishwa mwaka 2023 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanaonesha umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya uchunguzi na utoaji haki ili kukidhi mahitaji ya wakati uliopo.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia katika kushughulikia kesi za jinai yanahitaji umakini mkubwa, kwani kutokuzingatia taratibu sahihi kunaweza kuathiri uhalali wa ushahidi, haki za watuhumiwa na wananchi wengine wanaohusika katika mchakato wa haki.
Amesisitiza kuwa wataalamu wanapaswa kuitumia teknolojia kwa weledi na kuzingatia misingi ya sheria ili kuhakikisha maendeleo hayo yanasaidia kuongeza uwazi, usahihi na ufanisi katika upatikanaji wa haki, jambo linaloendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji katika Wizara hiyo, Jane Lyimo, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapa washiriki uelewa mpana kuhusu namna ya kukusanya, kuchambua na kuwasilisha ushahidi katika mazingira ambayo teknolojia imekuwa sehemu muhimu ya ushughulikiaji wa makosa ya jinai.
Lyimo amesema mabadiliko ya teknolojia yameongeza mahitaji ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi unaoendana na changamoto mpya za kiuchunguzi, hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za wizara kuboresha utendaji wa taasisi zinazohusika na mfumo wa haki jinai.
Ameongeza kuwa kuimarisha uwezo wa watendaji hao kutachangia kuboresha uchunguzi na uendeshaji wa mashauri huku ukizingatiwa wajibu wa kulinda haki za msingi za wananchi na kufuata sheria katika kila hatua ya mchakato wa utoaji haki.
