Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ,amewaagiza wenye leseni za uchimbaji madini kuzifanyia kazi kwa mujibu wa masharti yake, akionya kuwa Serikali itachukua hatua za kuzifuta iwapo masharti hayo hayatatekelezwa.
Makamu wa Rais ametoa onyo hilo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kusimamia katazo la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi. Ameitaka kampuni za ndani na nje kuwekeza katika viwanda vitakavyochakata madini hapa nchini hadi hatua ya bidhaa za mwisho. Amesema uwekezaji huo utapanua fursa za ajira, utatoa malighafi kwa viwanda na kuongeza mapato ya taifa.
Akitolea mfano dhahabu, Makamu wa Rais, amesema Tanzania inazalisha takribani tani 67 kwa mwaka na ina viwanda vinane vya kuongeza thamani ya madini hayo. Ametaja kupunguzwa kwa mrabaha wa dhahabu inayosafishwa nchini kutoka asilimia sita hadi nne kuwa miongoni mwa hatua zilizosaidia kuongeza mapato ya madini kutoka Sh bilioni 753.17 mwaka 2023/24 hadi Sh trilioni 1.39 mwaka 2025/26.
Makamu wa Rais amesema Serikali imeridhia kutenga asilimia 10 ya mapato ya madini kugharamia utafutaji wa madini kupitia Mfuko wa Utafiti wa Madini. ameilekeza Wizara ya Madini kusimamia matumizi ya fedha hizo ili tafiti zibaini maeneo mapya yenye madini na zipatie wawekezaji taarifa za kuaminika za jiolojia.
Akimkaribisha Makamu wa Rais kufungua mkutano huo, Waziri wa Madini Anthony Mavunde, amesema mkutano huo umevutia zaidi ya washiriki 1,700 kutoka Tanzania na nchi nyingine zikiwemo Kenya, Uganda, Madagascar, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana na Saudi Arabia. Amesema idadi hiyo ni kubwa zaidi tangu mkutano huo uanzishwe.
Akizungumzia mageuzi ya sekta ya madini katika miaka 10 iliyopita, Mavunde ametaja mchango mkubwa wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya sekta hiyo, ikiwemo kiwanda cha kutenganisha madini mazito yaliyomo kwenye mchanga kinajengwa wilayani Pangani, mkoani Tanga. Kiwanda hicho kinatarajiwa kupokea malighafi kutoka Pangani na Kigamboni, pamoja na Madagascar na Afrika Kusini. Aidha, maandalizi yanaendelea kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata niobiamu katika Bonde la Songwe, mkoani Mbeya.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), Victor Tesha, ameishukuru Serikali kwa kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo na kuwataka wanaoomba mikopo kuwasilisha mipango ya biashara inayotegemea tafiti za jiolojia.
Amesema taarifa kuhusu kiasi cha madini kilichobainishwa, muda wa uchimbaji na makadirio ya mauzo huisaidia benki kutathmini uwezo wa mchimbaji kurejesha mkopo. Aidha ameongeza kwamba baadhi ya vijana wamefanikiwa katika sekta hiyo kwa kupata mikopo ya benki, na kutoa wito wa kuanzishwa kwa shirikisho la wachimbaji wadogo la Afrika Mashariki na Kati ili kubadilishana ujuzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amewataka washiriki wafikie maazimio yanayoweza kutekelezwa na ambayo matokeo yake yanaweza kupimwa. Amesema Kamati inatarajia kuona miradi ikipata ufadhili na kuanza kutekelezwa, wachimbaji wakipata teknolojia na fursa za ajira zikiongezeka kwa Watanzania.
Katika Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi” Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhiwa tuzo maalumu ya mageuzi katika sekta ya madini iliyopokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi kwa niaba yake.

