Tanzania imeshiriki Mkutano Mkuu wa 179 wa Shirika la Kimataifa la Maonesho (BIE), uliofanyika tarehe 17 Novemba 2026 jijini Paris, Ufaransa. Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, akiambatana na Bw. Jonathan Nkwabi, Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Pembezoni mwa mkutano huo, Balozi Yakubu alikutana na Bw. Alain Berger, Rais wa Mkutano Mkuu wa BIE. Aidha, alimpongeza Bi. Albina Faria de Assis Pereira Africano, aliyemaliza utumishi wake kama Mwakilishi wa Angola katika BIE, kwa kutunukiwa Medali ya Dhahabu ya BIE, heshima ya juu zaidi ya shirika hilo. Tuzo hiyo inatambua mchango wake wa zaidi ya miongo miwili, ikiwemo kuongoza ushiriki wa Angola katika maonesho tisa ya kimataifa.
Ujumbe wa Tanzania ulipokea taarifa kuhusu maandalizi ya Expo 2030 Riyadh nchini Saudi Arabia, ikiwemo hatua za kuwawezesha washiriki wa kimataifa kujiandaa kwa maonesho hayo. Waandaaji wa Expo 2027 Belgrade nchini Serbia waliripoti kuwa ujenzi wa eneo la maonesho umefikia asilimia 85, huku waandaaji wa Expo 2027 Yokohama, maonesho ya kimataifa ya kilimo cha bustani nchini Japani, wakieleza maendeleo ya ujenzi wa mabanda na miundombinu kuelekea ufunguzi wa tarehe 19 Machi 2027.
Taarifa hizo zinaisaidia Tanzania kutambua mapema fursa za kutumia maonesho hayo kutangaza bidhaa za nchi, kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi wa kimataifa, kupanua masoko ya nje na kuvutia uwekezaji.

