
NA DENIS MLOWE, MBEYA
MPANGO wa Shule Salama unaotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), umeelezwa kuanza kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu, ikiwemo kuongezeka kwa ufaulu, kupungua kwa utoro na kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kutokana na changamoto mbalimbali zinazohatarisha usalama wao.
Hayo yameelezwa na Hilda Mgomapayo, Mratibu wa Mpango wa Shule Salama kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati wa kuhitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo watekelezaji wa mpango huo yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Kleruu mkoani Iringa
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii, wakuu wa shule, walimu wa malezi na unasihi, waratibu wa mpango pamoja na wenyeviti wa bodi za shule kuelewa majukumu yao katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira salama.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kutokea nyumbani, shuleni na katika jamii, huku ikiimarisha mifumo ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kupitia masanduku ya maoni na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto.
Mgomapayo amesema mafunzo hayo pia yamelenga kuimarisha huduma za ushauri na unasihi shuleni ili wanafunzi wanaokumbwa na changamoto mbalimbali wapate msaada wa kisaikolojia, waweze kujiamini, kueleza matatizo yao na kuendelea na masomo bila vikwazo vinavyoweza kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.
Amesisitiza kuwa ulinzi wa mtoto haupaswi kuishia katika kuhakikisha anapata elimu pekee, bali anapaswa kujengwa pia kimaadili ili aweze kujitambua, kujilinda na kuwa raia mwenye maadili mema na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Katika utekelezaji huo, amesema wenyeviti wa bodi za shule wana nafasi muhimu ya kuunganisha shule na jamii, huku maafisa maendeleo na ustawi wa jamii wakitakiwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu malezi chanya, ulinzi wa mtoto na umuhimu wa kushiriki katika shughuli za shule, ikiwemo kuchangia huduma ya chakula kwa wanafunzi.
Amesema mpango huo kupitia mradi wa SEQUIP ulilenga kufikia shule 2,000, lakini kutokana na juhudi za wasimamizi na wadau umeweza kufikia idadi inayozidi lengo hilo, huku akitoa wito kwa utekelezaji kuendelea kuimarishwa ili shule zote, za Serikali na binafsi, ziweze kunufaika kwa kuwa watoto wote wanahitaji mazingira salama ya kujifunzia.
Akizungumzia matokeo ya utekelezaji, Mgomapayo amesema takwimu za kipindi cha miaka mitatu zinaonesha kuongezeka kwa ufaulu na kupungua kwa utoro pamoja na wanafunzi wanaoacha shule, jambo alilolieleza kuwa ni ishara ya kuimarika kwa uelewa wa wanafunzi kuhusu haki zao, usalama na namna ya kujilinda dhidi ya vitendo hatarishi.
Kwa upande wake, Juma Mwishehe, mwalimu wa malezi na unasihi kutoka Shule ya Sekondari Luwalaje wilayani Chunya, amesema mafunzo hayo yamemwongezea uelewa wa namna ya kutambua, kuzuia na kushughulikia changamoto zinazowakabili wanafunzi kuanzia wanapotoka nyumbani hadi wanapofika shuleni.
Amesema miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili shule ni utoro na mimba za wanafunzi, akieleza kuwa baadhi ya shule zimekuwa zikikabiliwa na upungufu mkubwa wa wanafunzi kadiri wanavyopanda madarasa, hali inayohitaji ushirikiano wa walimu, wazazi na jamii katika kutafuta suluhisho.
Mwishehe ameongeza kuwa changamoto nyingine ni matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana katika baadhi ya maeneo, akisema walimu wanapaswa kushirikiana na wazazi kupitia umoja wa walimu na wazazi pamoja na jamii kutoa elimu na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujilinda dhidi ya vitendo hivyo.
Naye Ritah Mushi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa zaidi kuhusu wajibu wa maafisa maendeleo ya jamii katika kutoa elimu ya ulinzi wa mtoto na kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii pamoja na walimu kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanafunzi zinapatiwa ufumbuzi.
Mushi amesema amejifunza umuhimu wa kufuatilia usalama wa mtoto katika safari yake kutoka nyumbani kwenda shuleni, akieleza kuwa mtoto anaweza kuondoka nyumbani akiwa salama lakini akakumbana na vitendo vya ukatili au mazingira hatarishi akiwa njiani, hivyo jamii inapaswa kuwajibika kumlinda kila mtoto bila kujali kama ni mwanafunzi au la.
Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta mabadiliko katika jamii kupitia elimu ya malezi bora, ulinzi wa mtoto na ushiriki wa wazazi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma muhimu, ikiwemo chakula shuleni, ili waweze kuhudhuria masomo na kukamilisha mzunguko wao wa elimu wakiwa salama.
