Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Exim Tanzania imezindua kampeni ya miezi mitatu ya ‘Maliza Kirahisi Kidigitali-Kamata Kitita’, inayolenga kuhamasisha wateja kutumia huduma za kibenki za kidijitali katika miamala yao ya kila siku huku wakipata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali, ikiwemo zawadi kuu ya Sh milioni 15.

Kampeni hiyo itakayoendeshwa kuanzia Novemba 2026 hadi Februari 2027, ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuimarisha matumizi ya teknolojia na ubunifu katika utoaji wa huduma za kifedha, kwa kuwawezesha wateja kufanya miamala kwa urahisi, haraka na kwa uhakika bila kulazimika kutembelea matawi ya benki.

Huduma hizo zinapatikana kupitia njia mbalimbali za kidijitali zikiwemo Exim Pay, USSD \*150\*11#, Internet Banking, Exim WhatsApp Banking, Exim Wakala na Exim Mastercard, zinazowawezesha wateja kutuma fedha, kulipia bili, kununua umeme, kufanya manunuzi na kusimamia akaunti zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim Tanzania, Silas Matoi, alisema kampeni hiyo imeandaliwa kuwapa wateja fursa ya kunufaika na huduma za kidijitali pamoja na kujishindia zawadi za fedha taslimu.

Alisema kupitia droo za kila wiki, wateja 30 watajishindia Sh 50,000 kila mmoja, huku wateja 10 wakipata Sh 500,000 kila mmoja katika droo za kila mwezi.

Aliongeza kuwa katika droo kuu ya mwisho wa kampeni, washindi watatu watajishindia zawadi za Sh milioni tano, milioni 10 na milioni 15 kulingana na nafasi zao.

“Tunataka wateja wetu waweze kufanya miamala yao ya kila siku kwa urahisi kupitia njia mbalimbali za kidijitali. Tunawahamasisha kutumia huduma hizo na kutimiza vigezo vya kampeni ili waweze kujishindia zawadi,” alisema Matoi.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali katika shughuli za kila siku za wateja huku ikiwapa nafasi ya kuwania zawadi.

Alisema benki hiyo inawakaribisha wateja wote kushiriki kampeni hiyo kwa kutumia huduma zake za kidijitali na kutimiza vigezo vilivyowekwa.

“Tunawahamasisha wateja wetu kutumia huduma za Exim za kidijitali wanapofanya miamala yao ya kila siku. Pamoja na urahisi wanaoupata, wanapata pia fursa ya kuwania zawadi kupitia kampeni hii. Ujumbe wetu ni rahisi: Maliza Kirahisi Kidigitali-Kamata Kitita!” alisema D’souza.

Naye Afisa Mkaguzi wa Michezo ya Kubahatisha, Pendo Albert Mfuru, alisema droo za kampeni hiyo zitaendeshwa kwa mfumo wa kielektroniki unaochagua washindi kwa nasibu chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Alisema usimamizi huo unalenga kuhakikisha mchakato wa upatikanaji wa washindi unafanyika kwa haki na uwazi, huku washiriki wanaotimiza vigezo na masharti wakipata nafasi sawa ya kuwania zawadi.

“Tunathamini juhudi za kampuni zinazotoa promosheni zenye zawadi kwa wateja wao. Katika kampeni hii, tutasimamia mchakato wa droo ili kuhakikisha unafanyika kwa haki na uwazi,” alisema Mfuru.

Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Benki ya Exim Tanzania wa kuendelea kuimarisha huduma za kifedha zinazotumia teknolojia, huku ikiwahamasisha wateja kutumia njia zake za kidijitali kunufaika na urahisi wa kufanya miamala na fursa ya kujishindia zawadi.