Mpanda, Katavi
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mpanda imekamilisha ujenzi wa daraja la Mafunsi lenye urefu wa mita 20 linalounganisha kata ya Mwamkuru kutoka Manispaa ya Mpanda na kata ya Itenka iliyopo Halmashauri ya Msimbu mkoani Katavi.
Kukamilika kwa daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu kwa kata hizo ambazo ni maarufu kwa kilimo cha zao la mpunga mkoani humo kumeondoa changamoto ya muda mrefu ya kukosekana kwa kivuko katika mto Mafunsi hasa kipindi cha masika ambapo mtu huo hujaa maji.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Mpanda Mhandisi Simon Telephones amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi wa kata hizo ambao ni wakulima wakubwa wa mpunga walikuwa wanashindwa kusafirisha mazao yao kutoka upande mmoja wa mto kwenda upande wa pili.
“Walikuwa wanafika hapa na mazao yao yakiwa yamepakiwa kwenye trekta ilibidi washushe mizigo yao yote halafu waivushe mabegani mpaka upande wa pili kabla ya kuendelea na safari”.
“Aina hiyo ya usafirishaji ilikuwa inawapa gharama kubwa wananchi hao ila kwa sasa wanapita kwa urahisi na haraka bila kuingia gharama yeyote ile ya ziada na wanaona matunda ya serikali ya awamu ya sita”. amefafanua Mhandisi Telephones.
Kwa mujibu wa Mhandisi Telephones ujenzi wa daraja hilo la zege umehusisha ujenzi wa daraja kubwa sambamba na ujenzi wa madaraja mengine saidizi sita, ujenzi wa tuta la barabara ambalo linajumuisha ‘Gabion’, upandaji wa nyasi na ‘parapet’ za kingo za barabara.
Kwa upande wake Bw. Amos Juma mkazi wa kata ya Mwamkuru ameipongeza serikali kupitia TARURA kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo kwani kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wana mwamkuru wote pamoja na kata ya Itenka.
” Shughuli kubwa ya Mwamkuru ni kilimo na kilimo kinahitaji ukimaliza mavuno yanahitaji kusafirishwa ili yaweze kufika mjini kwenye masoko”.
“Kukosekana kwa daraja ilikuwa inatuwia vigumu sana kwetu kusafirisha mazao yetu kwenda mjini lakini kwa sasa hali ni nzuri kwani tunaweza kusafirisha mazao yetu wakati wowote iwe kiangazi au masika”. ameongeza Bw. Juma.

