Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ( wa pili kutoka kulia), akikagua mradi wa uboreshaji Bandari ya Mwanza Kaskazini, leo.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa( kulia) akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Mwanza Kaskazini kwa Waziri wa Uchukuzi..

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akisistiza jambo alipokagua uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa ( kulia) akimuongoza Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kukagua mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Mwanza Kaskazini.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa ( kulia) akimuonesha Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, jengo la abiria na mizigo (halipo pichani) kabla ya kukagua mradi huo wa uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Mwanza Kaskazini.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa habari,  baada ya kukagua mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini, leo.
……………

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

SERIKALI ya Awamu ya Sita imekamilisha asilimia 90 ya mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini, unaogharimu sh. bilioni 18.6 ni mkakati wa kuimarisha usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji, kukuza biashara na kuongeza ufanisi wa huduma za bandari.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alimetoa kauli hiyo jijini hapa leo, baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, akisema serikali imeweka kipaumbele katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kisasa ya bandari ili kutoa huduma bora, salama na endelevu kwa wananchi.

Alisema uboreshaji wa bandari hiyo umeleta mabadiliko makubwa katika uwezo wa kuhudumia meli na abiria, ikiwamo kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 kabla ya mradi hadi mita tano kwa sasa.

“Bandari ya Mwanza Kaskazini, uboreshaji umefikia asilimia 90. Kabla ya mradi huu unaogharimu sh. bilioni 18.6 kuanza, kina cha maji kilikuwa mita 3.5, leo kina cha maji ni mita tano. Gati lina uwezo wa kuegesha meli sita kwa wakati mmoja, ikiwamo meli ya MV Mwanza,” alisema.

Alisema mradi huo unahusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali, ikiwamo jengo la abiria, ghala la kuhifadhi shehena ya mizigo lenye uwezo wa tani zaidi ya 50, 000, ujenzi wa kingo za ziwa pamoja na upanuzi wa maeneo ya kuegesha meli na magari.

Profesa Mbarawa alisema, Bandari ya Mwanza Kaskazini ni kitovu cha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria, uboreshaji wake utaongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji na biashara ndani na nje ya nchi.

Alisema pia, serikali imeendelea kuboresha bandari za Kanda ya Ziwa kwa kutambua mchango wake katika kukuza uchumi, akitaja uwekezaji wa sh. bilioni 18.6 katika Bandari ya Mwanza Kaskazini, sh. bilioni 20.3 katika Bandari ya Kemondo na sh. bilioni 19.5 katika Bandari ya Bukoba.

Alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi hiyo kuwa, uwekezaji huo ni jitihada za kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini.

Alisema kukamilika kwa uboreshaji wa bandari hizo kutatoa fursa kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani kutumia usafiri wa majini kusafirisha bidhaa zao badala ya kutegemea malori pekee, hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza usalama wa abiria na mizigo.

MV MWANZA KUFUNGUA FURSA ZA BIASHARA

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alisema serikali imejenga meli ya kisasa ya MV Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 10, yakiwamo magari madogo.

Alisema meli hiyo inatarajiwa kutoa huduma katika Ziwa Victoria na kuunganisha Tanzania na nchi jirani za Kenya na Uganda ili kuongeza fursa za biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Alisema jengo jipya la abiria katika Bandari ya Mwanza Kaskazini lina uwezo wa kuhudumia watu 700 kwa wakati mmoja, tofauti na jengo la zamani lililokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 350.

“MV Mwanza tunataka iende nchi jirani za Kenya na Uganda, ili kukuza biashara na mataifa hayo na kuchangia uchumi wa nchi. TPA asilimia 90 tumemaliza, jengo la abiria litahudumia watu 700 kulinganisha na 350 wa jengo la zamani. Sasa simikeni maboya na minara ya kuongozea meli ziwe salama,” alisema.

Alisema asilimia kumi ya kazi zilizobaki kukamilisha mradi huo hazitakuwa kikwazo kwa meli hiyo kuanza kutoa huduma, baada ya kukamilika kwa gati, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) zitakutana kupanga ratiba za safari kwa kuzingatia mahitaji ya kibiashara na wananchi.

Aidha, alisema uwekezaji katika miundombinu ya bandari ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani wa kimataifa, hivyo sekta binafsi itumie fursa zilizopo kuwekeza katika sekta ya usafirishaji, ushiriki wake utasaidia kuongeza ufanisi, kupanua huduma na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mbossa, alisema mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini, ikiwamo kuongeza gati la kuhudumia shehena ya mizigo, umefikia asilimia 90 ya utekelezaji.

Alisema maboresho hayo yanayofanywa na serikali yataifanya bandari hiyo kutoa huduma zenye ushindani, kukuza biashara na kuongeza ufanisi katika kuhudumia abiria na shehena ya mizigo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.