Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo A. Saqware, amesema bima ni nyenzo muhimu katika kulinda wananchi, biashara na uwekezaji dhidi ya vihatarishi na hasara zinazoweza kujitokeza, hivyo kuchangia kujenga uchumi imara na unaostahimili misukosuko.

Amesema bima si huduma ya kifedha pekee, bali ni kinga inayowezesha watu binafsi na taasisi kuendelea na shughuli zao hata wanapokumbwa na majanga au changamoto zisizotarajiwa.

Dkt. Saqware ameyasema hayo wakati akizungumza katika kikao cha wahariri wa vyombo vya habari na TIRA, kilicholenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu majukumu na mchango wa mamlaka hiyo katika maendeleo ya Taifa.

Amesema TIRA ina jukumu muhimu la kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini kwa kuhakikisha kunakuwa na soko lenye uwazi, ufanisi, ushindani na linalolinda maslahi ya wateja pamoja na wadau wote.

Kwa mujibu wa Dkt. Saqware, sekta ya bima ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kulinda uwekezaji na biashara dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha hasara kubwa.

Amesema sekta hiyo pia inachangia kukuza uchumi jumuishi kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo, huku ikiimarisha uthabiti wa sekta ya fedha kupitia usimamizi imara wa soko la bima.

Aidha, amesema huduma za bima zinaongeza uhakika kwa wawekezaji na wajasiriamali, hivyo kuchochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini.

Alisisitiza umuhimu wa kujenga uelewa wa wananchi kuhusu huduma za bima, haki zao na namna ya kuzitumia ili kujikinga na athari za kiuchumi zinazoweza kutokana na majanga mbalimbali.

Dkt. Saqware amesema ukuaji wa sekta ya bima haupaswi kupimwa kwa ongezeko la kampuni au thamani ya biashara pekee, bali pia kwa kiwango ambacho wananchi na wafanyabiashara wanapata huduma, wanaelewa haki zao na kulipwa stahiki zao kwa wakati wanapopata hasara zinazolipika.

Akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari, amesema vina wajibu muhimu wa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima, aina za huduma zinazopatikana, haki za wateja na wajibu wa kampuni za bima.

Pia, amevitaka vyombo vya habari kuibua mijadala yenye tija kuhusu mafanikio na changamoto za sekta hiyo ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuchochea matumizi ya huduma za bima.

Amesema kwa ujumla, bima ni kinga ya uchumi dhidi ya vihatarishi na nyenzo ya kujenga uchumi imara na unaostahimili misukosuko, hivyo TIRA ina nafasi muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi shindani, jumuishi na ustahimilivu ifikapo mwaka 2050.