Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
TANZANIA inalenga kuwa kitovu cha uzalishaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia barani Afrika kupitia ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kuvutia wawekezaji katika eneo hilo.
Hatua hiyo inatokana na ahadi ya taasisi ya Sustainable Energy for All (SEforALL) ya kushirikisha sekta binafsi kuunda muungano wa wawekezaji utakaohamasisha uwekezaji katika teknolojia za nishati safi ya kupikia nchini.
Waziri wa Nishati, Juma Zuberi Homera, amesema hayo wakati akielezea matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki, ambako alishiriki Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam, leo Novemba 15, 2026, amesema ushirikiano huo ni miongoni mwa fursa zilizopatikana kupitia mazungumzo yaliyofanyika wakati wa mkutano huo, ambazo zinatarajiwa kuongeza uwekezaji na kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Amesema Tanzania pia imepata ahadi za ufadhili wa miradi ya nishati safi kutoka kwa washirika mbalimbali, ikiwamo Serikali ya Saudi Arabia, ambayo imeahidi kuendelea kufadhili miradi ya nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia.
Aidha, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha ufadhili wa majiko ya umeme 70,000, huku majiko mengine 70,000 yakitarajiwa kuidhinishwa hivi karibuni, hatua itakayochochea matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia.
Homera amesema taasisi ya International Solar Alliance (ISA) nayo imeahidi kushirikiana na Tanzania kuhamasisha matumizi ya nishati ya jua katika shule na vituo vya afya, pamoja na kutenga dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya miradi ya umeme wa jua katika nchi wanachama.
Amesema UK Aid imeahidi kutoa pauni milioni nne kwa ajili ya miradi ya nishati safi ya kupikia na nishati jadidifu, pamoja na kuwezesha wananchi kupata majiko ya umeme kupitia mfumo wa malipo ya awamu.
Ameongeza kuwa Wizara ya Nishati itaendelea na mazungumzo na taasisi hizo ili kuhakikisha ahadi za uwekezaji na ufadhili zinageuzwa kuwa miradi itakayochochea uzalishaji wa teknolojia za nishati safi na kuongeza upatikanaji wake kwa wananchi.
Wakati huo huo, amesema juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta hiyo zimeongeza idadi ya taasisi zinazotumia nishati safi ya kupikia kufikia 2,745, huku mitungi ya gesi 370,792 na majiko banifu 139,859 yakiwa yamesambazwa kwa wananchi.

