Na: OWM – TAMISEMI, Lindi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemueleza Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi jitihada alizozifanya za kukutana na Wakandarasi, Wahandisi Washauri, Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TARURA, Wakurugenzi wa Halmashauri na Waratibu wa Miradi ya TACTIC, ili kufuatilia na kuhimiza utekelezaji wa miradi ya TACTIC inayosuasua Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na maeneo mengine.
Prof. Shemdoe amemueleza Makamu wa Rais kuwa, Oktoba 3, 2026, jiji Dar es Salaam alifanya kikao kazi na wataalamu hao kuhimiza uwajibikaji kwa kufanya kazi usiku na mchana na kuwashauri wakandarasi wasio na uwezo mkubwa wa kifedha kuhakikisha wanatoa mikataba midogo (sub-contract) kwa wakandarasi wengine wenye uwezo wa kukamilisha kazi kwa wakati.
“Mhe. Makamu wa Rais nilikuja hapa Lindi nikatoa maelekezo kwa wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji, na nikaamua kuwaita katika kikao kazi cha kuhimiza uwajibikaji jijini Dar es Salaam cha Wakandarasi wote, Wahandisi Washauri, Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TARURA, Wakurugenzi wa Halmashauri na Waratibu wa Miradi ya TACTIC,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amempongeza Mhe. Prof. Shemdoe kwa jitihada za kumhimiza mkandarasi KIKIM Contractors Limited na mbia wake AMACO Enterprises kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa TACTIC Manispaa ya Lindi, unaohusisha ujenzi wa Soko Kuu la Matopeni, Stendi ya Mabasi Mitwero na barabara zenye urefu wa kilomita 5.3, ili wananchi wanufaike na mradi huo wa Ustawishaji Miji Tanzania (TACTIC).
Mhe. Ndejembi ametoa pongezi hizo Novemba 14, 2026, akiwa Manispaa ya Lindi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 19 unaolenga kuboresha mazingira ya biashara, huduma za kijamii na usafirishaji, pamoja na kuongeza mapato ndani ya Manispaa ya Lindi.
“Wanalindi, nampa maua yake Prof. Shemdoe kwa jitihada zake za kuwahimiza wakandarasi hawa wanaosuasua, licha ya kufikia asilimia 24 ya utekelezaji wa mradi,” ameeleza Mhe. Ndejembi.
Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, akijibu maombi ya Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Mhe. Mohamedi Mussa Utaly, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais, amesema Serikali inaleta Shilingi Milioni 600 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nangaru, huku mwaka wa fedha ujao ikitenga fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Kitumbikwela.
Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais kuhusu ujenzi wa barabara ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Prof. Shemdoe amesema amewaelekeza wataalamu wa TARURA kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili itengewe fedha katika mwaka wa fedha 2027/28.
Aidha, Prof. Shemdoe amemshukuru Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kuielekeza TAKUKURU na Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mkandarasi KIKIM Contractors Limited na mbia wake AMACO Enterprises kwa kushindwa kukamilisha kwa wakati Mradi wa TACTIC Manispaa ya Lindi, unaohusisha ujenzi wa Soko Kuu la Matopeni, Stendi ya Mabasi Mitwero na barabara zenye urefu wa kilomita 5.3.

