Na: OWM–TAMISEMI, Nanyamba – Mtwara

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu katika eneo linalozunguka Mradi wa Kimkakati wa Kongani la Viwanda Maranje ili kuwa kitovu cha uzalishaji katika Mkoa wa Mtwara na ukanda wa kusini.

Mhe. Ndejembi amesema hayo leo Novemba 13, 2026, akiwa katika Kijiji cha Maranje, Halmashauri ya Mji Nanyamba, alipoutembelea na kuuzindua mradi wa Kongani la Viwanda Maranje ulioanzishwa kwa lengo la kujenga eneo maalumu la uwekezaji na viwanda vya kubangua korosho na kusindika bidhaa mbalimbali zinazotokana na korosho pamoja na mazao mengine ya kilimo.

“Serikali Kuu inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa kuweka mkazo katika ujenzi wa miundombinu wezeshi katika eneo hili ili liweze kuwa kitovu cha uzalishaji kitakachobadilisha korosho kutoka zao la biashara ya malighafi na kuwa chanzo kikubwa cha viwanda, ajira, kipato na maendeleo ya wananchi,” amesisitiza Mhe. Ndejembi.

Ili kutimiza azma hiyo ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, alipopewa fursa na Makamu wa Rais kueleza mkakati wa kutekeleza maelekezo yake ya ujenzi wa barabara katika mradi huo, amesema mara baada ya kupokea maelekezo hayo alimtaka Meneja wa TARURA Mkoa wa Mtwara kuwasilisha andiko la mpango wa ujenzi wa barabara katika eneo la mradi huo.

Akizungumzia ombi la Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Mhe. Arif Suleiman Premji, la ujenzi wa barabara ya Nanguruwe–Mkunwa yenye urefu wa kilomita 17, Prof. Shemdoe amesema kilomita 5 zimeshakamilika kwa kiwango cha lami na itaendelea kujengwa kwa kuongeza kilomita 1.5 kwa kila mwaka.

Utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara, umeme na bomba la gesi utawezesha uzalishaji wa zaidi ya ajira 35,000 za moja kwa moja zinazotarajiwa kupatikana katika viwanda, maghala, usafirishaji, uendeshaji wa mitambo, ulinzi, biashara na huduma mbalimbali.