Na Sixmund Begashe, Arusha

FARU ni moja ya urithi adimu na adhimu nchini na ana mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi na pia yupo katika kundi la wanayamapori walio hatarini kutoweka hatua inayoilazimu Serikali kuja na mpango kabambe wa kumlinda. 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha wataalam wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha, chenye lengo la kutoka na Mpango mpya wa Usimamizi na Uhifadhi wa faru nchini kwa Mwaka 2027/2037.

Dkt. Lobora amesema Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mhifadhi namba moja, imeweka jitihada kubwa kwenye uhifadhi wa wanyamapori hususani faru, hivyo lengo la Mpango huo mpya ni kuongeza idadi zaidi ya faru nchini. 

Ameongeza kuwa Mpango huo utasaidia kuongeza idadi ya faru kutoka idadi ya sasa ambayo ni zaidi ya faru 250 na kufikia zaidi ya faru 600 katika kipindi cha miaka 10 ijayo. 

“Ili tufikie lengo ni lazima tulinde makazi yao, tuwalinde faru wenyewe, tuwe na wataalam wa kutosha, tunatumia teknolojia ya kisasa, pamoja na uratibu madhubuti chini ya Wizara yetu ya Maliasili na Utalii,” alifafanua Dkt. Lobora.

Aidha, Dkt. Lobora amewapongeza wataalam hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuandaa Mpango huo huku akiwataka kuhakikisha unakamilika mapema ili uanze kutumika kama ilivyokusudiwa. 

Naye Mratibu wa Faru Taifa Bw. Philbert Ngoti, amesema kuwa maandalizi ya mpango huo yamefikia zaidi ya asilimia 70 hivyo wanatarajia kupitia kikao hicho kilichowashirikisha wataalam kutoka taasisi za uhifadhi wa wanyamapori utakamilika. 

Bw. Ngoti ameongeza kuwa ili kupata mpango ulio bora zaidi timu hiyo ya wataalam imemshirikisha nguli wa Uhifadhi wa Spishi Prof. Noah Sitati kuwawezesha wataalam hao kutokana na taaluma na uzoefu wake kitaifa na kimataifa.