Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amewahimiza wananchi wa Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara kutumia huduma ya umeme kama nyenzo ya kuongeza uzalishaji, kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao, badala ya kuutumia kwa matumizi ya mwanga pekee.
Ameyasema hayo Novemba 12, 2026, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, mkoani humo ambapo alieleza hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Nishati katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini.
“Umeme usitumike katika kuwasha taa pekee, bali utumike katika shughuli za kiuchumi zitakazomwezesha kila mwananchi kujenga uchumi wake,” amesema Mhe. Salome.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme vijijini, Mhe. Salome amesema Serikali imekamilisha kazi ya kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini huku akibainisha kuwa bado kuna baadhi ya vitongoji katika maeneo ya Mangaka ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.
Ameeleza kuwa vitongoji hivyo vimejumuishwa katika mpango wa utekelezaji wa mradi maalumu unaolenga kuhakikisha wananchi wote waliobaki wanapata huduma ya umeme, hatua itakayochochea shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi katika maeneo hayo.
Aidha, Mhe. Salome amemshukuru Makamu wa Rais kwa kumpa nafasi ya kueleza maendeleo ya sekta ya nishati katika ziara yake iliyoanzia mkoani Ruvuma huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia pia maelekezo ya viongozi wakuu kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa nishati na kuchochea maendeleo ya wananchi.

