MASASI – MTWARA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ameonya kuwa Serikali haitamvumilia afisa ugani, afisa kilimo au mfanyabiashara atakayebainika kuchakachua pembejeo na kuwanyonya wakulima wa korosho.
Akizungumza na wananchi wa Masasi mkoani Mtwara, Makamu wa Rais amesema ruzuku ya pembejeo inayotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wakulima, hivyo haitaruhusiwa kugeuzwa njia ya watu wachache kujitajirisha.
Onyo hilo limetolewa kufuatia kushuka kwa uzalishaji wa korosho kutoka tani 600,000 hadi tani 400,000, huku wakulima wakilalamikia pembejeo kutotoa matokeo yaliyotarajiwa.
Makamu wa Rais amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani, uzalishaji ulikuwa tani 180,000 kabla ya kuongezeka hadi tani 600,000 baada ya Serikali kuweka ruzuku ya pembejeo ya salfa.
Ameitaka Wizara ya Kilimo kuchunguza malalamiko kuhusu ubora wa pembejeo, yakiwemo madai ya kuchakachuliwa au kupungua nguvu kutokana na kukaa muda mrefu, ili kubaini chanzo cha kushuka kwa uzalishaji.
Aidha, amewahimiza wakulima kuendelea kwenda mashambani, akiwahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ruzuku na kushughulikia changamoto za pembejeo ili uzalishaji urejee katika kiwango cha awali na hatimaye kufikia tani milioni moja.
Akieleza hatua zinazochukuliwa, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema salfa ya unga haikutosheleza mahitaji katika msimu huu, hali iliyolazimu kuletwa kwa salfa ya maji ambayo haikufanya vizuri katika baadhi ya maeneo.
Amesema awali kulikuwa na takribani tani 16,000 za salfa ya unga na baadaye zikaongezwa tani 10,000, lakini mahitaji yalikuwa makubwa zaidi.
Chongolo amesema timu ya wataalamu kutoka TPHPA, TARI na Wizara ya Kilimo imepelekwa kufanya uchunguzi wa kina kubaini iwapo changamoto ilitokana na viuatilifu, namna ya matumizi au sababu nyingine.
Ameahidi kuwa katika maandalizi ya msimu ujao, wizara inalenga kuhakikisha salfa ya unga inafika katika maeneo ya uzalishaji ifikapo Machi mwaka ujao ili wakulima waipate kwa wakati.
Amesisitiza kuwa pembejeo za ruzuku ni nyenzo ya kuwakwamua wakulima kiuchumi, na kuwaonya wanaotaka kuzitumia kujinufaisha kwa kuwaumiza wananchi.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Masasi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amepongeza uwekezaji wa Serikali katika elimu, afya na miundombinu, akisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya hiyo.
Akizungumzia suala la maji, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amekiri kuwapo kwa pengo kubwa la huduma, akisema mahitaji ya Masasi ni lita milioni 16, wakati kiasi kinachofikishwa ni lita milioni sita, hivyo kuacha upungufu wa lita milioni 10.
Amesema Wizara ya Maji itatoa fedha za dharura kwa hatua za haraka, huku timu ya wataalamu ikishirikiana na Serikali ya Mkoa, viongozi wa Masasi na wananchi kuandaa ufumbuzi wa muda mfupi na mpango wa kudumu.
Waziri huyo ameahidi kuisimamia kazi hiyo kwa haraka, sambamba na maandalizi ya mradi mkubwa utakaokidhi mahitaji ya wananchi wa Masasi kwa muda mrefu.

