Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Madaba wakati akiwa Ziarani mkoani Ruvuma
…………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amemwagiza Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, kuhakikisha mbolea ya ruzuku inapatikana kwa bei elekezi ya Serikali katika Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, pamoja na maeneo mengine ya mkoa huo, kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya pembejeo hiyo muhimu.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo, Novemba 10, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mtyangimbole–Dabaga, wenye thamani ya shilingi bilioni 5.6, ambao umefikia asilimia 96 ya utekelezaji na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 19,000 katika vijiji vitatu.
Katika ziara hiyo, amekagua matenki ya kuhifadhia maji na miundombinu mingine ya mradi, pamoja na kuzungumza na wananchi waliopata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili.
Akizungumzia upatikanaji wa mbolea, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali haiwezi kukubali wananchi kuuziwa mbolea ya ruzuku kwa bei inayozidi ile iliyoelekezwa, huku akimtaka Waziri wa Kilimo kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu sababu za kupanda kwa bei hiyo.
Amesisitiza kuwa bei elekezi ya Serikali lazima izingatiwe Madaba na maeneo mengine, ili wakulima wanufaike na ruzuku inayotolewa kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.
Aidha, akizungumzia bei ya mahindi kwa mwaka 2026, Ndejembi amewahimiza wakulima kujiandaa na msimu ujao wa kilimo kwa kuongeza uzalishaji, akieleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mbolea ya ruzuku inapatikana na changamoto za masoko na bei ya mahindi zinashughulikiwa ili wakulima wasipate hasara.
Kuhusu Mradi wa Maji wa Mtangimbole–Dabaga, Makamu wa Rais amesema utekelezaji wake ni kielelezo cha namna Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyoendelea kupeleka huduma muhimu karibu na wananchi na kuboresha maisha yao.
Amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi mmoja mmoja, hususan katika maeneo ya vijijini.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa kulinda misitu, kupunguza ukataji miti ovyo na kuhifadhi vyanzo vya maji, akionya kuwa uharibifu wa mazingira unachangia mabadiliko ya tabianchi, ukame na kupungua kwa upatikanaji wa maji.
Ziara hiyo imeweka msisitizo katika dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo yanayoonekana, huku changamoto zinazogusa maisha ya wananchi, hususan wakulima, zikishughulikiwa kwa wakati.

