Na Jeremia Mwakyoma & David Kavindi 

Picha na Godfrey Mwiliko & Jeremiah Mbwambo

DODOMA – NOV 11, 2026

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inatarajia kunufaika kwa kupata msaada mkubwa wa vifaa tiba vya kisasa kutoka kwa shirika la Human Bridge la nchini Sweden. Manufaa haya yanatokana na ziara ya Uongozi wa BMH nchini Sweden Mwezi Septemba 2026 iliyoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo. 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi wakati alipopokea ujumbe wa Viongozi Wawakilishi wa Taasisi hiyo waliyotembelea BMH kujionea hali ya utoaji huduma na kuzungumzia mashirikiano baina ya taasisi hizo mbili.

“Mashirikiano baina ya BMH na shirika la Human Bridge la nchini Sweden linalojihusisha na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kutoka nchini humo na kusambaza kwenye maeneo yenye uhitaji yatainufaisha BMH na tayari tumeshawasilisha orodha ya awali ya vifaa ambavyo BMH tunahitaji kwa ajili ya kupata msaada huo kutoka Human Bridge” alifafanua Prof. Makubi

Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe kutoka Sweden yalipo Makao Makuu ya shirika hilo Bw. Robert Bergman pamoja na kushukuru ushirikiano kutoka BMH, alibainisha kuwa shirika hilo lina uzoefu wa miaka mingi katika nyaja ya upatikanaji na usambazaji vifaa tiba, limefanya kazi na nchi nyingi na kwa hapa Tanzania kwa muda mrefu limekuwa likisambaza vifaa kwenye Hospitali za Wilaya.

” Tumeshafanya kazi na Hospitali nyingi za Wilaya zinazomilikiwa na Serikali zikiwemo za Wilaya za Arumeru, Serengeti, Bunda, Kiomboi, Mkalama, Chemba, Mufindi, Geita na Chato, Aidha, eneo jingine la Mashirikiano litakuwa kujengeana uwezo kwa upande wa ufundi na matengenezo ya vifaa tiba kwa wataalamu wa BMH” aliongeza Bw. Bergman .

Ujumbe huo wa Human Bridge ulipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali.