Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki ya CRDB, Maregesi Shaaban akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Happy Lazaro, Arusha
Arusha .Benki ya CRDB imesema imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 4.3 kwa ajili ya kuchochea uwekezaji katika sekta ya kilimo, hususani mazao ya bustani (Horticulture), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji na kukuza mnyororo wa thamani wa mazao nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki ya CRDB, Maregesi Shaaban amesema benki hiyo imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kufadhili sekta ya kilimo, hususani mazao ya bustani (horticulture) .
Maregesi ameyasema hayo leo katika jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.
Mageresi amesema kuwa,benki hiyo imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kupitia utoaji wa mikopo na huduma mbalimbali za kifedha.
Amesema mikopo inayotolewa na benki hiyo katika sekta ya kilimo inachangia asilimia 45 ya uwekezaji na mikopo yote inayotolewa na taasisi za fedha nchini, hatua inayoonesha mchango wa CRDB katika kuendeleza sekta hiyo.
“Maonesho hayo yamewakutanisha wakulima, wawekezaji, wanunuzi wa mazao na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo, pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.”amesema Maregesi .
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuvutia uwekezaji na kuweka mazingira bora ya kukuza kilimo, huku akibainisha kuwa CRDB imejipanga kutoa huduma za kibenki zitakazowawezesha wawekezaji kutumia fursa zilizopo nchini.
Amefafanua kuwa,kupitia ushiriki wake kama mdhamini mkuu wa HortiLogistica Africa 2026, benki hiyo imetoa huduma mbalimbali za kibenki katika maonesho hayo, zikiwemo huduma za amana, malipo na elimu kuhusu mikopo ili kuwasaidia wadau kuelewa fursa za kifedha zinazopatikana.
Ameongeza kuwa sekta ya kilimo nchini imeanza kupiga hatua katika matumizi ya teknolojia za kisasa za uzalishaji, pamoja na kuongeza thamani ya mazao kupitia uchakataji na ufungashaji unaozingatia viwango vya kimataifa badala ya kuyauza yakiwa ghafi.
Maregesi amefafanua kuwa,CRDB inaendelea kupanua shughuli zake nje ya Tanzania, ikiwa na uwepo nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na kufungua ofisi Dubai kwa lengo la kuimarisha huduma zake katika masoko ya kimataifa na kuunganisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema benki hiyo imepata ithibati ya Mfuko wa Kimataifa wa Tabianchi (Green Climate Fund – GCF), kupitia ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia masuala ya mazingira, na kufanikiwa kupata ufadhili wa dola milioni 200 za Marekani kwa ajili ya uwekezaji katika uzalishaji wa mazao ya chakula.
Amesema fedha hizo zitasaidia kuimarisha uzalishaji wa chakula na kukuza uwekezaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira, huku akiishukuru Serikali kwa kuwezesha ushirikiano huo na kuwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

