Na, Mwandishi Wetu – Nairobi, Kenya
TANZANIA imesisitiza dhamira yake ya kuunga mkono Mpango wa Dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa kukabiliana na mvua zinazotarajiwa za El Niño, huku ikihimiza nchi wanachama kuimarisha ushirikiano, kubadilishana taarifa kwa wakati na kuchukua hatua za pamoja ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi, miundombinu na shughuli za kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Prof. Palamagamba Kabudi wakati wa Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Kisekta wa kujadili maandalizi na hatua za pamoja za kukabiliana na mvua hizo, uliofanyika Nairobi, Kenya Novemba 06, 2026.
Mhe. Mmuya alieleza kuwa majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi hayaishii katika mipaka ya nchi moja, hivyo nchi wanachama wa EAC zinapaswa kushirikiana katika kukabiliana na hatari hizo na kuimarisha uwezo wa ukanda wa Afrika Mashariki wa kudhibiti athari zake.
Alibainisha kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, ufuatiliaji wa hali ya hewa, tathmini ya maeneo hatarishi na utoaji wa elimu kwa umma, pamoja na kuboresha mifumo ya kukabiliana na dharura.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. James Millya, uliridhia Mpango huo wa Dharura wa EAC wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño (EAN-PREP), unaolenga kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama katika utoaji wa tahadhari za mapema na kukabiliana na athari zake katika sekta muhimu kama vile afya, miundombinu, kilimo, na usalama wa chakula.
Sekretarieti ya EAC imetakiwa kuhakikisha kuwa inatafuta rasilimali za utekelezaji wa mpango huo na kuimarisha ushirikiano na IGAD pamoja na taasisi za utabiri wa hali ya hewa za kitaifa.

