Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea na juhudi za kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wadau kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea hatua hiyo muhimu katika Jumuiya.
Katika hatua hiyo, Wizara iliwashirikisha Waheshimiwa Wabunge kutoka Kamati tano za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo ni Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU); Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii; na Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.
Zoezi hilo lililofanyika Novemba 4, 2026, lilifunguliwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb.), kwa niaba ya Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu. Lengo lilikuwa kuwajengea Wabunge uelewa kuhusu dhana ya Fungamano la Kisiasa la EAC, misingi yake, pamoja na hatua zilizofikiwa katika zoezi hilo.
Aidha, elimu hiyo inalenga kuwawezesha Wabunge na wadau wengine kubainisha masuala muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika Rasimu ya Katiba hiyo, ili waweze kutoa maoni na mapendekezo yatakayochangia kuboresha rasimu wakati wa mchakato rasmi wa ukusanyaji wa maoni utakapoanza.
Ushirikishwaji wa Wabunge na makundi mbalimbali ya kijamii ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha mchakato huo unakuwa shirikishi na jumuishi, huku wananchi wakipata taarifa sahihi na fursa ya kushiriki katika kujadili mustakabali wa ujumuishaji wa kikanda na mwelekeo wa EAC kuelekea Fungamano la Kisiasa.
Ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki uliongozwa na Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya.

