Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya,akizungumza kwenye kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Arusha. 

 Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TIRA, Ponziano Rusiano Lukosi akizungumza kwenye kiako hicho jijini Arusha

Washiriki wa kikao kazi hicho wakifuatilia mada mbalimbali jijini Arusha. 

……………. 

Happy Lazaro, Arusha

Arusha .Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kuondoa vikwazo vinavyochelewesha ulipaji wa fidia za bima na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha wadau wa sekta ya bima Kanda ya Kaskazini jijini Arusha, Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema ulipaji wa fidia ndiyo kipimo muhimu cha imani ya wananchi kwa sekta ya bima.

Amesisitiza kuwa bima haipaswi kuishia katika kukusanya malipo ya awali, bali lazima itimize wajibu wake wa kumlinda mwananchi pale anapokumbwa na janga.

Dkt. Lupilya amependekeza kuanzishwa kwa ‘Mfumo wa Kitaifa wa Uratibu wa Madai ya Bima (National Insurance Claims Coordination Framework)’ utakaounganisha kampuni za bima na taasisi muhimu, ikiwemo Jeshi la Polisi, hospitali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wadau wengine, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuharakisha maamuzi ya madai.

Ameeleza kuwa mfumo huo utasaidia pia kuboresha takwimu za madai yaliyolipwa, yaliyocheleweshwa na yale yenye viashiria vya udanganyifu, huku akisisitiza umuhimu wa kila taasisi kutekeleza wajibu wake na kutoa taarifa kwa wakati.

Dkt. Lupilya amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya bima hayapimwi kwa idadi ya watu wanaokata bima pekee, bali pia kwa kasi, uwazi na haki katika kulipa fidia pale wanapohitaji huduma hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TIRA, Ponziano Rusiano Lukosi, amebainisha changamoto zinazochangia migogoro ya madai, zikiwemo magari kuwekewa bima bila ukaguzi wa kutosha, makadirio yasiyo halisi ya gharama za matengenezo na ucheleweshaji wa taarifa za uchunguzi wa ajali.

Naye Mchunguzi Mwandamizi wa TAKUKURU Arusha, Julieth Mwambola, amewataka wananchi kuripoti vitendo vya rushwa vinavyohusiana na ufuatiliaji wa madai ya bima kupitia namba ya bure 113, huku akizihimiza kampuni za bima kutoa taarifa za viashiria vya udanganyifu.

Kikao kazi hicho kimewakutanisha kampuni za bima, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, LATRA, NHIF, wawakilishi wa gereji, mawakala wa bima na taasisi nyingine zinazoshiriki katika mnyororo wa kushughulikia madai ya fidia.