Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imekamilisha maandalizi ya awali ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dumila, wenye urefu wa kilomita 66, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha 220/33kV katika eneo la Dumila, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro.

Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Mhe. Sara Msafiri Ally, aliyetaka kujua lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho na laini ya umeme, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema kuwa hatua inayofuata ni kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Mhe. Makamba ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umepangwa kuanza baada ya kukamilika kwa miradi ya awamu ya kwanza ya Gridi Imara.

Kwa upande mwingine, Mhe. Salome amebainisha kuwa baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mvomero yana hali ya unyevunyevu mwingi kutokana na mazingira yake, hali inayochangia nguzo za miti kuoza na kuanguka. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imepeleka zaidi ya nguzo 156 za zege kwa ajili ya kuboresha uimara wa miundombinu ya usambazaji umeme na kupunguza changamoto ya kuanguka kwa nguzo.