Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema miradi ya maji ya Uwiro, Kikatiti–Samaria na Imbaseni katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2026/27 na kunufaisha wananchi zaidi ya 37,861.

Miradi hiyo ni sehemu ya jumla ya miradi nane ya maji inayotekelezwa wilayani humo kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 9.1, ikiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo husika.

Akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Samwel Nassari, aliyetaka kujua lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi ya maji ya Uwiro, Imbaseni, Kikatiti na Samaria, Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso alisema utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea kwa hatua tofauti.

Waziri huyo alisema kazi zinazotekelezwa kupitia miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa vyanzo vya maji (intakes), ujenzi na ukarabati wa matanki nane yenye jumla ya ujazo wa lita milioni tatu, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 51.2 pamoja na ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji.

Alisema miradi ya Uwiro na Kikatiti–Samaria imefikia wastani wa asilimia 40 ya utekelezaji kwa kila mradi, huku mradi wa Imbaseni ukiwa umefikia asilimia 80.

“Mheshimiwa Spika, miradi ya Uwiro na Kikatiti–Samaria imefikia wastani wa asilimia 40 za utekelezaji kila mmoja wakati mradi wa Imbaseni ukiwa umefikia wastani wa asilimia 80,” alisema Waziri huyo.

Aliongeza kuwa Serikali imepanga kukamilisha miradi yote hiyo ndani ya mwaka wa fedha 2026/27 ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma ya maji kwa uhakika.

Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Arumeru na kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa matumizi ya nyumbani na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.