Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog,Dodoma
JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatarajia kutumia miundombinu ya Tanzania kusafirisha madini ya lithium kwenda katika masoko mbalimbali, kupitia bandari ya Kigoma na Bandari ya Dar es Salaam, kufuatia ujenzi wa bandari mpya upande wa nchi hiyo katika Ziwa Tanganyika.
Waziri wa Ujenzi wa DRC, John Lunda, amesema kuwa bandari hiyo inatarajiwa kuanza kufanya kazi Machi 2027, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa madini hayo na kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Amesema kuwa tayari nchi hizo zinaendelea na maandalizi ya kuunganisha shughuli za bandari hizo, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuboresha mfumo wa usafirishaji wa bidhaa na kuunganisha miundombinu ya mataifa hayo.
Aidha, Lunda amesema kuwa DRC inaendelea kujifunza kutoka Tanzania katika sekta ya miundombinu, akitaja Reli ya Kisasa ya SGR na maendeleo ya miundombinu ya kitaifa na kimkoa kuwa miongoni mwa maeneo aliyoyashuhudia wakati wa ziara yake Dodoma.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa DRC, Judith Tuluka, amesema kuwa nchi yake inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Tanzania katika masuala ya usalama, miundombinu na maendeleo.
Amesema kuwa ziara yake ya Dodoma imempa fursa ya kujifunza namna Tanzania ilivyopanga na kujenga Mji wa Serikali wa Mtumba, maarifa ambayo amesema yanaweza kusaidia katika upanuzi na uboreshaji wa mji mkuu wa Kinshasa.
Pia ameongeza kuwa DRC inatambua ushirikiano unaotolewa na Tanzania katika masuala ya usalama, huku akieleza kuwa ziara hiyo imehusisha pia ukaguzi wa eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania.
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, amesema kuwa Tanzania na DRC zina fursa nyingi za kushirikiana katika sekta za uchumi, ikiwemo madini ya lithium na kilimo cha zabibu, ambapo Dodoma imewekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao hayo.
