Na Sophia Kingimali, Dar es Salaaam
Katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) 2026, wasichana wameongoza kwa idadi ya watahiniwa waliofaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C, wakifikia 527,622 ikilinganishwa na wavulana 443,254, licha ya wavulana kuwa na asilimia kubwa ya ufaulu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Prof. Said Mohamed, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitangaza matokeo ya mtihani huo, akieleza kuwa ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 3.42 na kufikia asilimia 85.22 kutoka asilimia 81.80 mwaka 2025.
Amesema kwa kuzingatia asilimia ya ufaulu, wavulana waliongoza kwa kufikia asilimia 86.18, huku wasichana wakipata asilimia 84.43, hata hivyo kundi la wasichana lilikuwa na idadi kubwa ya waliofaulu kutokana na kuwa na watahiniwa wengi zaidi waliofanya mtihani.
Amesema ufaulu wa wasichana umeongezeka kwa asilimia 3.22 kutoka asilimia 81.21 mwaka 2025, huku wavulana ukiongezeka kwa asilimia 3.67 kutoka asilimia 82.51 ya mwaka huo.
Prof. Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 1,168,718 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 637,214 sawa na asilimia 54.52 na wavulana 531,504 sawa na asilimia 45.48.
Amesema kati yao, watahiniwa 1,139,318 sawa na asilimia 97.48 walifanya mtihani, wakiwemo wasichana 624,976 sawa na asilimia 98.08 na wavulana 514,342 sawa na asilimia 96.77.
Ameongeza kuwa watahiniwa 29,400 sawa na asilimia 2.52 hawakufanya mtihani huo, wakiwemo wavulana 17,162 sawa na asilimia 3.23 na wasichana 12,238 sawa na asilimia 1.92.
Katika ubora wa ufaulu, alisema watahiniwa 429,667 sawa na asilimia 37.72 walipata madaraja ya A na B, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.82 ikilinganishwa na mwaka 2025.
Amesema kwa upande wa jinsia, wasichana waliopata madaraja hayo waliongezeka hadi asilimia 34.27 kutoka asilimia 33.71, huku wavulana wakifikia asilimia 41.90 kutoka asilimia 40.73 mwaka jana.
Kuhusu ufaulu wa masomo, alisema Kiswahili kimeongoza kwa kupata asilimia 93.13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.56, kikifuatiwa na Uraia na Maadili kilichopata asilimia 90.12, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.75.
Amesema Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi kilipata asilimia 76.53, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.24, Hisabati asilimia 62.56, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.90, huku English Language ikipata asilimia 50.50, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.39.
Hata hivyo, amesema ufaulu wa somo la Sayansi na Teknolojia umeshuka kwa asilimia 4.09 na kufikia asilimia 80.34, huku ubora wa ufaulu wa madaraja ya A na B ukishuka hadi asilimia 33.60 kutoka asilimia 48.14 mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, alisema NECTA imezuia matokeo ya watahiniwa 371 waliougua na kushindwa kufanya mtihani katika masomo mengi au yote, huku wakipewa fursa ya kurudia mtihani mwaka 2027.
Amesema Baraza pia limefuta matokeo ya watahiniwa 31, wakiwemo 26 waliobainika kufanya udanganyifu na watano walioandika lugha ya matusi katika hati zao za majibu.
Kuhusu upatikanaji wa matokeo, Prof. Mohamed alisema yatatolewa bila majina ya watahiniwa kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi, hivyo namba za mtihani zitatumika kuwatambua watahiniwa.
Amesema matokeo hayo yanapatikana kupitia tovuti za www.necta.go.tz, www.moe.go.tz na www.tamisemi.go.tz, huku Baraza likiyawasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari.
